Latest Posts

WAZIRI MKUU MAJALIWA ATOA WITO UMOJA WA MATAIFA KUUNGA MKONO MATAIFA YASIYO NA UWEZO KIUCHUMI

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kusaidia mataifa madogo yenye changamoto za kiuchumi ili yaweze kuboresha mipango yao ya ndani.

Ameyasema hayo jioni ya siku ya Jumapili, Septemba 22, 2024 wakati akiwasilisha salamu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye ufunguzi wa Mkutano wa siku mbili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kujadili Hatma ya Siku Zijazo (Summit of the Future) ulioanza siku hiyo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani.

Akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79), Waziri Mkuu Majaliwa alieleza juhudi za Tanzania katika masuala ya uchumi, ulinzi, na mabadiliko ya tabianchi.

Kuhusu uchumi, Majaliwa aliomba Umoja wa Mataifa kusaidia mataifa yasiyo na uwezo ili yatekeleze mipango yao ya kiuchumi. Alieleza kuwa Tanzania imepanga kuimarisha sekta ya kilimo, uwekezaji, viwanda, madini, na maliasili kwa ajili ya kujenga mustakabali bora kwa wananchi wake.

Majaliwa pia alisisitiza umuhimu wa usalama, akibainisha kuwa ustawi wa taifa lolote hauwezi kufikiwa bila amani na ulinzi, si tu ndani ya mipaka yake bali pia kwa nchi jirani.

“Unapozungumzia ujenzi wa kesho iliyobora kwa watu wako, huwezi kufanikiwa kama hakuna nchi iliyo salama; kwa hiyo ulinzi na usalama ni suala la muhimu na tumeihakikishia jumuiya ya kimataifa kwamba pamoja na ulinzi wa ndani bado ulinzi kwa nchi jirani nao pia wa muhimu,” ameongeza.

Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Waziri Mkuu alionya juu ya athari zinazoshuhudiwa duniani, ikiwemo ukame na mafuriko, na kueleza kuwa Tanzania inahamasisha wananchi kujadiliana namna ya kukabiliana na changamoto hizo huku wakifanya shughuli zao za kiuchumi.

Pia alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti kupunguza uzalishaji wa hewa chafu, kulinda bayoanuwai, na kusaidia nchi zinazoendelea kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Awali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alieleza kuwa mkutano huo umeitishwa ili kutafuta mbinu za kuikomboa dunia na kuirejesha kwenye njia sahihi, akibainisha kuwa dunia inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo migogoro ya kijiografia, vitisho vya kinyuklia, na uwekezaji katika silaha za kisasa badala ya maendeleo.

“Niliitisha kikao hiki kwa sababu changamoto za karne ya 21 zinahitaji kutatuliwa na majibu ya karne ya 21 kwa kupitia mifumo ambayo imeundwa vema, iliyo jumuishi na inayohitaji utaalamu wa watu wote.”, alisema.

Waziri Mkuu Majaliwa aliambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Thabit Kombo, Waziri wa Nchi (OR-Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo, na Naibu Waziri wa Afya wa SMZ, Nassor Ahmed Mazrui. Kaulimbiu ya mkutano huo ni “Hakuna kuachwa nyuma: Kushirikiana kuendeleza amani, maendeleo endelevu, na heshima ya binadamu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.”

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!