Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahimiza Watanzania kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapokutana na bidhaa zisizo rasmi, ambazo zinaweza kuwa zimeagizwa kutoka nje, kuzalishwa, au kusambazwa nchini bila kibali.
Ametoa wito huo Alhamisi Agosti 29, 2024, Bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Hai, Saasisha Mafue kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu. Mbunge Mafue alitaka kujua hatua gani Serikali inachukua kudhibiti uingizaji holela wa pombe kali, ambao unachangia vijana kulewa sana nyakati za mchana.
“Serikali ina utaratibu wa kutambua na kudhibiti uzalishaji na uingizaji wa vileo nchini kwa kutoa vibali vya biashara kwa wasambazaji. Aidha, tunaendelea kutoa elimu juu ya madhara ya ulevi uliopitiliza ili kuwalinda vijana wetu,” amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu pia ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuwahamasisha vijana kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali, na kwamba utaratibu huo umewezesha vijana wengi kupata kipato na kuboresha hali za maisha zao na za familia zao.
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha sheria na taratibu za uingizaji, uuzaji, na usambazaji wa bidhaa ili kuhakikisha kila kinachoingizwa nchini kinakidhi viwango vya afya vya Watanzania.
Ametoa wito kwa jamii kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa za utengenezaji wa bidhaa zisizoidhinishwa ambazo zinaweza kuwa na madhara makubwa, hususan vileo vikali.
“Ni muhimu taasisi zote zinazojihusisha na masuala ya vijana zitoe elimu ya ujasiriamali, kuwafundisha maadili mema, na kuwapa stadi za maisha ili kuhakikisha vijana wanajiepusha na tabia mbaya,” ameongeza.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameelezea hatua za Serikali katika kuboresha huduma za afya nchini, akisema kuwa uwekezaji mkubwa umefanywa ili kuhakikisha hatua za awali za utambuzi wa mama mjamzito zinaweza kubaini uwezekano wa mtoto kuzaliwa na ulemavu.
Ameeleza kuwa tafiti za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa hatua za awali zinaweza kupunguza ulemavu kwa zaidi ya asilimia 80, na kwamba huduma hizo sasa zinapatikana kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali za kitaifa.