Serikali imeombwa kuangalia namna ya kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu kutumia mifumo ya mitandao ili nao waweze kunufaika na fursa ya mikopo inayotarajiwa kuanza kutolewa na Halmashauri nchini kote mwezi huu.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Foundation for Disabilities (FDH), Michael Salali, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu harakati za taasisi hiyo kushiriki katika kudhibiti vitendo vya ukatili kwa watu wenye ulemavu kupitia mradi waliowezeshwa na Women Fund Tanzania Trust.
Salali amesema kuwa pamoja na mapinduzi makubwa ya matumizi ya mitandao, kundi la watu wenye ulemavu lipo nyuma katika matumizi ya teknolojia kutokana na changamoto mbalimbali zinazotokana na aina za ulemavu walionao.
“Kwa mfano, mwenye ulemavu wa ukiziwi anategemea lugha ya alama, hivyo taarifa zinamchelewa kumfikia. Vilevile, ndugu zetu wasioona wanakutana na vikwazo wanapotaka kuingia kwenye mifumo hiyo ya mitandao,” amesema Salali.
Ameongeza kuwa changamoto nyingine ni kwamba mitandao hiyo mara nyingine hutumiwa vibaya, ambapo watu wenye ulemavu wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili kupitia majukwaa hayo.
Akizungumzia mikopo ya asilimia kumi inayotarajiwa kutolewa na Halmashauri, Salali amesema kuwa pamoja na kwamba hatua hiyo inakaribishwa kwa furaha, bado kuna kikwazo cha teknolojia ambacho kinaweza kuwakwamisha wenye ulemavu kunufaika na mikopo hiyo.
“Serikali imeunda mfumo wa kuomba mikopo mtandaoni, lakini bado kuna changamoto kubwa kwa watu wenye ulemavu ambao hawana uwezo wa kuingia kwenye mifumo hiyo. Tunataka tuwajengee uwezo ili waweze kutumia mfumo huo na kufaidika na mikopo hiyo,” amesisitiza.
Salali ameonya kuwa, ikiwa wenye ulemavu hawatawezeshwa kutumia mfumo huo, itakuwa sawa na ukatili kwao kwani itawanyima fursa ya kupata mikopo hiyo inayolenga kuinua maisha yao.
Aidha, amesema kuwa taasisi yake imeandaa mpango wa kukutana na viongozi wa Halmashauri kote nchini ili kuona namna ya kusaidia makundi ya wenye ulemavu kwa kuweka mikakati stahiki itakayowawezesha kunufaika na mikopo hiyo.
“Tunataka tuwajengee uwezo ili waweze kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo na kuhakikisha kuwa wanazitumia kwa malengo sahihi, ili waweze kurejesha mikopo hiyo na wengine pia wapate nafasi ya kunufaika,” amesema Salali.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuwajengea wenye ulemavu uwezo wa matumizi bora ya mikopo hiyo ili kuwawezesha kuboresha maisha yao na kujikwamua kutoka kwenye umasikini.
Salali amewahimiza watu wenye ulemavu wasijinyanyapae na badala yake wachangamkie fursa zinazopatikana, huku akiitaka jamii kutowabagua au kuwafanyia vitendo vya ukatili. Amehimiza ushirikiano wa jamii katika kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanapata haki sawa na fursa sawa katika masuala yote ya kijamii.
Shirika la FDH, kwa kushirikiana na Women Fund Tanzania Trust, limekuwa likitoa mafunzo kwa watu wenye ulemavu katika Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, kuwaelimisha jinsi ya kukabiliana na vitendo vya ukatili na hatua zinazopaswa kuchukuliwa iwapo vitendo hivyo vitatokea.
“Tunataka kuona ushiriki wa watu wenye ulemavu katika nyanja mbalimbali kama vile uongozi, ili nao waweze kuleta mabadiliko katika jamii yetu,” amehitimisha Salali.