Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa msaada wa ufadhili kutoka Mfuko wa Ireland limetoa msaada wa pikipiki 12 kwa Serikali ya Tanzania ili kuboresha maeneo ya ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko , pamoja na ufuatiliaji wa tetesi za matukio yenye athari kwa afya ya binadamu kwenye jamii .
Akipokea pikipiki hizo siku ya Jumamosi Agosti 17, 2024 katika Ofisi za WHO Jijini Dodoma Gerald Manasse kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Idara ya afya amesema pikipiki hizo zitagawiwa kwenye halmashauri 12 ambazo zinatokana na mikoa saba ya Tanzania bara.
“Baada ya kuwa tumefanya tathimini ya takwimu tukaona mikoa na halmashauri ambazo mara nyingi zinakutwa na milipuko ya magonjwa, kwa hiyo tukaona ni vizuri tuwasaidie hizi pikipiki ili kuwawezesha na kuwapa urahisi wa kuweza kusafiri wanapokwenda kufuatili matukio haya ya magonjwa”, amesema Manasse.
Aidha, Manasse amesema kwa mikoa ya pembezoni ambayo ina maeneo magumu kufikika pikipiki hizo zitarahisisha mikoa hiyo kufikika kwa uharaka na kwaurahisi.
‘’Ni pikipiki nzuri ambazo tuliwasiliana na Mamlaka ya usafirishaji kwa maana ya wizara ya ujenzi wakatupatia vigezo na viwago tulipaswa kupata pikipiki ambazo zinaweza kuvumilia hali ya vijijini”, ameeleza.
Pamoja na hayo Manasse amesema watahakikisha pikipiki hizo zinatumika ipasavyo kulingana na malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka mfuko wa Ireland Margaret Gaynor ameishukuru Serikali kupitia Tamisemi na wizara ya afya kwa ushirikiano mzuri na kuweka mifumo mizuri na endelevu katika kutatua changamoto za afya kwa wananchi wa Tanzania.