Ijumaa ya Septemba 6 mwaka 2024 kwenye viwanja vya Kilombero, Mkuu wa Wilaya ya Arusha mkoani Arusha Felician Mtahengwa anatarajia kuzindua rasmi msimu mpya wa ugawaji wa fedha za mikopo ya vijana, wanawake na wenye ulemavu wa wilayani Arusha.
Zoezi hilo ambalo awali lilipangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu, linahusisha takribani Shilingi bilioni 6 na milioni 300 ambazo zimetolewa na serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mtahengerwa amewaambia wanahabari kuwa katika uzinduzi huo, kutatolewa elimu mbalimbali juu ya uundaji wa vikundi vya wajasiriamali, elimu ya uombaji mikopo, namna ya kuandika maandiko ya kibiashara pamoja na namna wajasiriamali wanavyoweza kukuza mitaji yao.
Uzinduzi wa ugawaji wa fedha hizo za mikopo isiyo na riba limeahirishwa na ofisi ya Mkuu wa wilaya baada ya kueleza kuwa amepokea maombi mengi kutoka kwa wawezeshaji wa mafunzo na wananchi wa Arusha, waliotaka zoezi hilo kusogezwa mbele ili kupata nafasi ya kujiandaa zaidi kuchangamkia fursa hiyo ya fedha za mkopo kutoka serikalini.