Wizara ya Afya nchini Tanzania imeeleza kupokea taarifa za tetesi za uwepo wa ugonjwa wa Marburg katika Mkoa wa Kagera na kuchukua hatua za haraka kufanyia kazi taarifa hizo.
Katika taarifa iliyotolewa, Januari 15, 2025, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, amesema Wizara imetuma timu ya wataalamu kufanya uchunguzi wa kina, kuchukua sampuli, na kuzifanyia vipimo vya maabara ili kubaini ukweli wa suala hilo.
“Hadi sasa, majibu ya uchunguzi wa kimaabara kutoka kwa wahisiwa wote waliochukuliwa sampuli hayajathibitisha uwepo wa virusi vya Marburg,” amesema Waziri Mhagama.
Ameongeza kuwa Wizara ya Afya imeimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa katika maeneo yote nchini na itaendelea kutoa taarifa sahihi kwa wananchi na jumuiya ya kimataifa, ikiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO).
Aidha, Waziri amewatoa hofu wananchi, akiwahakikishia kuwa serikali inachukua hatua madhubuti kuhakikisha usalama wa afya ya jamii. Ameomba wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kiafya na kufuata maelekezo ya mamlaka husika.
Serikali inasisitiza kuwa itatoa taarifa zaidi pindi uchunguzi utakapokamilika au iwapo kutakuwa na maendeleo mapya katika suala hilo.