Latest Posts

WIZARA YA KATIBA NA SHERIA WAHITIMISHA KAMPENI YA UTOAJI ELIMU YA UTAWALA BORA NA URAIA MARA

Wizara ya Katiba na Sheria imehitimisha rasmi kampeni maalum ya utoaji wa elimu ya uraia na utawala bora katika Mkoa wa Mara, baada ya kutembelea wilaya zote za mkoa huo. Kampeni hiyo ilihusisha mafunzo kwa kamati za usalama, wakurugenzi, na wakuu wa idara mbalimbali za halmashauri, huku ikisisitiza matumizi ya elimu hiyo katika kuboresha utendaji wa kazi.

Akizungumza wakati wa hitimisho la kampeni hiyo wilayani Bunda, Wakili wa Serikali Mkuu, Joyce Mushi, amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwa mwanga kwa watendaji wa serikali katika utekelezaji wa majukumu yao. Alibainisha kuwa kampeni hiyo imefanyika kwa mafanikio makubwa, na matarajio yao ni kuona elimu hiyo ikileta mabadiliko chanya kwa jamii ya Mkoa wa Mara na kusaidia kufanikisha utekelezaji wa 4R za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Tumetoa mwanga na tumewafungua. Niwaombe viongozi wa Wilaya ya Bunda, ambapo tumekamilisha zoezi hili, mkayatumie mafunzo haya kikamilifu. Hatutarajii kuona mambo yakienda tofauti, nasi tutajitahidi kufuatilia hili,” amesema Joyce Mushi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dkt. Vincent Naano, ameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kutoa elimu hiyo muhimu, na ametoa wito wa mafunzo hayo kushushwa hadi kwa watumishi wa ngazi za chini, wakiwemo wenyeviti wa vijiji, makatibu tarafa, na madiwani. Amesisitiza kuwa elimu ya utawala bora itasaidia kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

“Kazingatieni mlichofundishwa na katumieni taaluma mliyopata kutatua kero za wananchi. Hatutarajii kuona migongano; mkizingatia utawala bora, changamoto katika maeneo yenu zitapungua kwa kiasi kikubwa,” amesema Dkt. Naano.

Kampeni hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha watendaji wa umma wanazingatia utawala bora, uwajibikaji, na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!