Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Felister Mdemu amesema kuwa, Wizara inatambua kuwa kuna changamoto mbalimbali katika uratibu ikiwemo ya ufinyu wa bajeti ya kufanya ufuatiliaji wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
Naibu Katibu Mkuu huyo ameyasema hayo Jumatano Septemba 4, 2024 wakati akizungumza katika ufunguzi wa Mafunzo Ya Wajumbe Wa Baraza la Taifa Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) na Wasajili Wasaidizi yaliyofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete.
Amesema changamoto nyingine ni pamoja na ukosefu wa mafunzo ya mara kwa mara kuhusu Sheria, Kanuni na Miongozo ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na mafunzo ya mfumo wa Kieletroniki wa usajili na uratibu (NIS).
“Kwa hiyo , Wizara imeamua kuandaa mafunzo haya ili kuwapitisha katika Sheria,Kanuni na Miongozo, mfumo wa Kieletroniki wa usajili na uratibu (NIS) maana mfumo huu umefanyiwa mabadiliko hasa baada ya kuongezewa kipengele cha Ramani ya Kidigitali”, Amesema Mdemu
Aidha amesema, kutokana kuboreshwa kwa mfumo wa Kieletroniki wa usajili na uratibu (NIS) baadhi ya taarifa zitahitajika kuhuishwa katika mfumo huo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika hayo Mwantumu Mahiza amewataka Wasajili kufanya kazi kwa karibu na NGOs kwenye maeneo yao na kufuatilia shughuli wanazofanya kwa mustakabali wa nchi ya Tanzania.