Katika kuadhimisha Wiki ya Maji, Wizara ya Maji imetoa mchango wa Shilingi milioni 20 kwa ajili ya matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza Ijumaa, Machi 21, 2025, wakati wa kukabidhi mchango huo kwa ajili ya matibabu ya watoto watano, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amesema wameguswa na changamoto za magonjwa ya moyo, hasa baada ya mmoja wa wafanyakazi wa wizara hiyo kufariki ghafla kwa tatizo hilo.
“Tunatengeneza wataalamu lakini ghafla mtaalamu anakutoka kwa sababu ya changamoto ya moyo ambayo haikugundulika mapema. Tumejipanga kuhakikisha wataalamu wetu wa sekta ya maji wanapimwa afya zao ili kuepuka madhara kama haya,” amesema Mhandisi Waziri, akimwakilisha Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.
Aidha, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika huduma za matibabu ya moyo na kusisitiza umuhimu wa taasisi nyingine za sekta ya maji kushirikiana katika kuhakikisha wafanyakazi wanapata huduma za afya ya moyo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Anjela Muhozya, amesema kuna changamoto ya upatikanaji wa huduma za moyo katika mikoa mingi nchini, jambo linalosababisha watoto wengi kugunduliwa na matatizo ya moyo wakiwa wamechelewa.
“Kwa sasa tunafanya huduma za Tiba Mkoba wa Mama Samia ili kuwafikia wananchi wa mikoani mapema na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya katika mikoa hiyo ili waweze kugundua matatizo ya moyo kwa watoto mapema,” amesema Dkt. Muhozya.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Everlasting Lyaro, ameeleza kuwa mchango huo ni mwanzo wa ushirikiano wa muda mrefu kati ya Wizara, DAWASA na JKCI. Amefichua kuwa mamlaka hiyo ipo katika hatua za mwisho za kuandaa Hati ya Makubaliano (MoU) kwa ajili ya programu ya kupima afya za wafanyakazi wake.
“Mwaka ujao tunatarajia kudhamini matibabu ya watoto zaidi ya 10. Kila mmoja wetu ni mzazi, tunapowaona watoto hawa wenye changamoto za moyo tunafikiria pia watoto wetu na wa ndugu zetu,” amesema Lyaro.
Akizungumzia kuhusu hali ya magonjwa ya moyo kwa watoto, Dkt. Stella Mongella, Daktari Bingwa wa Magonjwa Moyo kwa Watoto JKCI ameeleza kuwa katika kila vizazi hai 100, mtoto mmoja anazaliwa akiwa ana shida kwenye moyo huku kwa Tanzania ambayo imejaliwa takribani vizazi hai milioni 2 kila mwaka, takribani watoto 20000 kila mwaka huzaliwa wakiwa na shida kwenye moyo.
“Kati ya hao watoto 20000, takribani 4000 wanahitaji matibabu kwa dharura ikiwa ni matibabu yanayohitaji ndani ya mwaka wa kwanza wa maisha yao. Idadi ya watoto wanaozaliwa na shida kwenye moyo ni endelevu hivyo kuongeza ukubwa wa matatizo ya moyo kwa watoto”.