Latest Posts

YERICKO NYERERE WA CHADEMA AMTETEA ABDUL DHIDI YA TUNDU LISSU

Na; mwandishi wetu

Mjumbe wa Mkutano mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutoka Kigamboni, Dar es Salaam Yericko Nyerere ameendelea kumshukia vikali Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara Tundu Lissu kwa kudai kuwa amekuwa ni kiongozi muongo na anayependa kuwashushia tuhuma ‘nzito’ viongozi na wanachama wenzake majukwaani ili tu ajijenge na kunufaika yeye kisiasa jambo ambalo si la kiungwana

Kupitia chapisho lake aliloweka kwenye mitandao yake binafsi ya kijamii, Yericko Nyerere ametolea mfano tuhuma za ‘mabilioni ya Abdul’ ambayo mara zote Lissu amekuwa akituhumi viongozi wenzake ndani ya chama hicho kufikiwa na ‘mabilioni’ hayo na kutengeneza mianya ya rushwa ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini, tuhuma ambazo Yericko anasema kuwa ni za uongo na za kupuuzwa

Amesema licha ya kwamba Tundu Lissu kwa nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Bara kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili lakini mara zote hajawahi kuitisha kikao wala kushughulikia jambo hilo zaidi ya kwenda hadharani kinyume na Katiba ya chama hicho

Yericko ameendelea kufafanua kuwa moja ya miiko ya Kikatiba kwenye chama hicho ni kwamba mtu au watu wanaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa adhabu yake ni kufukuzwa uanachama

“Sasa baada ya kelele zake kuwa nyingi chama kiliamua kuingilia kati, kikamtaka aeleze ndani ya vikao akashindwa kueleza kwa ushahidi, ndipo mmoja wa viongozi waandamizi (Ezekia Wenje, Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Viktoria na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho) akaomba kukifafanulia chama kuhusu undani na ukweli wake hiki kinachoitwa rushwa ya Abdul kwa viongozi wa CHADEMA” -Yericko

Anasema mbele ya wajumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA na mbele ya Lissu, kiongozi huyo alifafanua kwamba yeye kama mfanyabiashara na mtu maarufu nchini ana urafiki wa karibu na Abdul (mtoto wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, aitwaye Abdul Hafidh Amir), na kwamba kwa kuwa Lissu alikuwa akiilalamikia sana serikali kwamba pesa yake ya matibabu hajalipwa, na kwa kuwa hilo ni haki yake kwa mujibu wa kanuni za Bunge, hivyo inaelezwa kuwa kiongozi huyo aliona ni vyema akazungumza na Abdul ili asaidie ‘kusukuma’ serikali imlipe Lissu hela zake

Inaelezwa baada ya mawasiliano hayo, Abdul aliuliza endapo Lissu ana nyaraka za kuthibitisha madai hayo, na alipojibiwa kuwa anazo ikamlazimu kiongozi huyo ampigie simu na kumueleza kwamba kuna mtu anayeitwa Abdul ambaye anaweza kusaidia ‘kusukuma’ kupatikana kwa stahiki zake

“Wakapanga miadi (ahadi) wakutane wote nyumbani kwa Lissu, wakamkuta akiwa na msaidizi wake bwana Djumbe hivyo kikao kikawa cha watu wanne, ambapo Abdul alimuomba Lissu nyaraka zake zote za madai ya matibabu na akamwambia azitume kwa email, zikatumwa, kikao kikaisha kiongozi yule na Abdul wakaondoka zao) -Yericko

“Sasa wiki kadhaa baadaye wakati mchakato wa malipo hayo ukiendelea chini ya Abdul, Lissu akagundua kiongozi yule aliyempeleka Abdul kwake amemgeuka, hamuungi mkono kwenye ajenda zake kadhaa mbeleni, Lissu akaamua kumzushia kwamba kiongozi huyo aliyempeleka Abdul kwake ili amuhonge mamilioni ya pesa, na kwamba ana ushahidi wa CCTV camera za kikao, ndio akaamini amemshika pabaya kwa kuwa ana video za kikao ambazo kwa ujanja wame-mute sauti” -Yericko

Aidha, Yericko Nyerere anasema kashfa hiyo iliwaunganisha viongozi wengine wengi ndani ya chama hicho akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Taifa ambaye pia anagombea tena kutetea nafasi hiyo Freeman Mbowe  kwa madai ya kwamba amehongwa (amepokea rushwa), ingawa bahati mbaya ni kwamba Lissu alituma pia nyaraka zake kwa njia za email, jambo ambalo ni ushahidi tosha kwamba kikao chao kilihusu nyaraka hizo na si vinginevyo

Pia, Yericko Nyerere ameendelea kulidadavua suala hilo kwa kudai kuwa kiongozi huyo anayetuhumiwa na Lissu alieleza yote hayo kwa ushahidi wa wazi, na kwamba baada ya kiongozi huyo kumaliza kuongea, wajumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA waliokuwepo kwenye kikao hicho walimgeukia Lissu kujibu hoja hizo lakini katika hali ya kushangaza Lissu akakataa kata kata kujibu badala yake alisema yeye alishatolea maelezo jambo hilo

Yericko amehitimisha kwa kusema kwa sasa hoja ya ‘mabilioni ya Abdul’ haipewi kipaumbele na Lissu, na kwamba mijadala yake mingi amekuwa akikwepa kuzungumzia kwa undani suala hilo kutokana na kile alichodai kuwa uongo wake umebainika, “sasa mtu wa aina hii anawezaje kuwa Mwenyekiti wa chama Taifa?, mimi sitampa kura yangu”

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!