Latest Posts

ZAIDI YA MITI 250 YAPANDWA KULINDA CHANZO CHA MAJI MTO MAHULULU MVOMERO

Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu, kwa kushirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Mvomero pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wamefanikisha zoezi la upandaji wa miti zaidi ya 250 katika chanzo cha maji cha Mto Mahululu. Zoezi hilo ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akiongoza zoezi hilo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mvomero, Saidy Nguya, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Maulid Dotto, ametoa wito kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa vyanzo vya maji kuacha kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo ili kulinda vyanzo vya maji na kuepuka changamoto ya upungufu wa maji siku zijazo.

Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Ofisi ya Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu, ambao ndio wasimamizi wa vyanzo vikuu vya maji, Magrethi Phati, ameushukuru uongozi wa Wilaya ya Mvomero pamoja na wananchi kwa ushirikiano wanaoendelea kutoa katika juhudi za utunzaji wa vyanzo vya maji. Aidha, amewaomba wananchi kuendelea kushirikiana na bodi hiyo katika kulinda vyanzo vya maji, hatua itakayosaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Naye Mhifadhi wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Mvomero, Medison Nilahi, amewahimiza wananchi kutumia kipindi cha masika kupanda miti, akibainisha kuwa TFS ipo tayari kutoa miche ya miti bure kwa wananchi kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi wa mazingira.

 

 

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!