Latest Posts

ZAIDI YA VIJANA 1000 WAPATIWA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI NA FURSA ZA KIMATAIFA MOROGORO

Zaidi ya vijana 1,000 kutoka mkoani Morogoro wakiwemo wanafunzi na wahitimu wa vyuo vikuu, vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) wamepatiwa mafunzo ya kiuchumi, kijamii na kivitendo kupitia Kongamano la Nje ya Box Youth Talk 2025, lililoandaliwa na Taasisi ya Ufaulu Project.

Akizungumza katika kongamano hilo mkoani Morogoro, Mei 10, 2025, Mkurugenzi wa Ufaulu Project, Simon Chammy, amesema lengo kuu la kongamano ni kuwafundisha vijana maarifa ambayo hawapati kupitia mfumo rasmi wa elimu, ili kuwasaidia kutambua na kutumia fursa zilizopo ndani na nje ya nchi kujiajiri au kuajiri vijana wenzao.

Amesema wamejikita katika kuwajengea vijana uwezo wa kuiona elimu kama nyenzo ya kubadili maisha kwa vitendo, hasa katika sekta kama kilimo, ufugaji na ujasiriamali.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Masuala ya Mazingira na Kilimo, Josephat William, amewahimiza vijana kuchangamkia fursa za ubunifu katika sekta ya mazingira, hasa katika kuunda teknolojia na suluhisho la changamoto za mabadiliko ya tabianchi kama vile ukame na magonjwa yanayoathiri mazao.

Amesema mabadiliko ya tabianchi si tishio tu bali ni fursa ya kuleta suluhisho na uvumbuzi mpya, na vijana ndio walengwa wakuu katika mapinduzi hayo ya kijani.

Pia, Inspekta Gerald Mwasambili kutoka Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Morogoro, ametoa elimu kwa vijana kuhusu taratibu za kupata hati ya kusafiria (passport) na namna sahihi ya kufuata viza katika balozi husika, ili kufanikisha safari zao za kitaaluma, ajira au biashara nje ya nchi.

Mmoja wa washiriki, Ester Moses, amesema amehamasika na elimu ya uwekezaji na utunzaji wa fedha aliyopata kwenye kongamano hilo, jambo ambalo awali halikuwa sehemu ya maarifa yake shuleni. Ametoa shukrani kwa waandaaji wa Ufaulu Project kwa kuwapa vijana maarifa ya maisha.

Kongamano hili limedhihirisha kuwa ubunifu, elimu ya vitendo na ufahamu wa fursa nje ya mfumo rasmi vinaweza kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya vijana nchini Tanzania.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!