Latest Posts

ZOEZI LA USAFI LA JUMAMOSI LAIMARISHWA JIJI LA DAR ES SALAAM

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka viongozi wa Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha kuwa mitaa yote 159 na kata 26 zinashiriki kikamilifu katika zoezi la usafi wa mazingira ili kulifanya Jiji hilo kuwa safi, salama na la kuvutia kwa wageni na wakazi wake.

Mpogolo ametoa agizo hilo mara baada ya kushiriki zoezi la usafi lililofanyika katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo, likiwemo eneo la fukwe za Dengu, kwa kushirikiana na wananchi pamoja na makampuni ya usafi. Zoezi hilo ni sehemu ya utaratibu wa usafi wa kila Jumamosi.

“Usafi ni jukumu la kila mmoja wetu, na kila kiongozi aliyeomba dhamana ya kuongoza anapaswa kuonyesha mfano. Taka nyingi zinazofika kwenye fukwe zinatoka mitoni, jambo ambalo linadhihirisha uzembe wa baadhi ya maeneo,” alisema Mpogolo.

Amesema ni wajibu wa kila kiongozi kuhakikisha maeneo wanayoyaongoza yanakuwa safi, hasa wakati huu ambapo mvua zimeanza kupungua, na kutoa fursa kwa utekelezaji wa shughuli za usafi kwa ufanisi zaidi.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kuweka mpango wa kudumu wa kufanya usafi kwenye fukwe za Bahari ya Hindi, hasa eneo la Dengu na Feri, ambayo yamekuwa yakipokea taka kwa wingi kutokana na uchafu unaosafirishwa kupitia mito.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Faraja Nakua, amesema kuwa kwa kushirikiana na wadau wa usafi, jiji limeanzisha mkakati endelevu wa kufanya usafi kila wiki kwa kuweka vifaa na vitendea kazi katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya kuboresha mazingira ya mji.

“Tutaendelea kuboresha hali ya usafi kwa kushirikiana na wananchi. Zoezi hili ni endelevu na tunalenga kulifanya liwe sehemu ya utamaduni wa wakazi wa Dar es Salaam,” alisema Nakua.

Mpango huo wa usafi unalenga si tu kutunza mazingira bali pia kuwavutia watalii na wageni wanaoingia jijini kupitia maeneo ya fukwe, ambayo ni vivutio muhimu vya kiuchumi na kijamii.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!