Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu ameagiza kuwepo kwa mazingira rafiki kati wafanyabiashara na taasisi za Kiserikali, ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Akizungumza na waandishi wa habari, muda mfupi baada ya kukagua mabanda mbalimbali katika Tamasha la Kariakoo, katika viwanja vya Mnazi mmoja, Zungu amesema Rais Dkt. Samia Sauluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kusisitiza mahusiano bora kati ya wafanyabiashara na TRA hivyo fursa hiyo itumike kujenga na kuinua uchumi.
Katika hatua nyingine, Zungu amezitaka taasisi zinazohusika na wafanyabiashara ikiwemo TBS na TRA kutumia muda mwingi kutoa elimu kwa wafanyabiashara badala ya kukamata bidhaa zao.
“Nia ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wafanyabiashara wanakuwa na mazingira rafiki katika kufanya kazi kwao, hivyo furasa hii itumike kuboresha mahusiano yenu,” alisema Zungu na kuongeza;
“Taasisi kama TBS, TRA na nyinginezo zitumike zaidi katika kufanya kazi za wananchi kwa kutoa elimu badala ya kukaa tu ofisini na kukamata bidhaa zisizokidhi viwango,”
Katika hatua nyingine, Zungu alimpigia simu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Abdul Katunzi na kumtaka afike katika maonesho hayo pamoja na timu yake ili kutoa elimu kwa wafayabiashara walipo viwanjani hapo.
“Nadhani mlipata barua ya kujulishwa uwepo wa tamasha hili la maonesho hapa Mnazi Mmoja, hivyo mfike hapa kwa ajili ya kutoa elimu zaidi kwa wafanyabiashara badala kuliko kuwakamata tu pale wapokosea katika uuzaji wa bidhaa zao,” alisikika Zungu katika mazungumzo yake na Mkurugenzi wa TBS, kwa njia ya simu.
Kilele cha tamasha hilo kinatarajiwa kufanyika Jumamosi hii, Septemba 21, 2024 huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Seleman Said Jafo.