Latest Posts

JENERALI MUHOOZI KAINERUGABA AAMUA KUTOGOMBEA URAIS MWAKA 2026, ASEMA ATABAKI JESHINI

Na Amani Hamisi Mjege.

Mkuu wa Majeshi wa Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ametangaza rasmi kuwa hatagombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2026, isipokuwa ataelekeza nguvu zake jeshini huku akimuunga mkono baba yake, Rais Yoweri Museveni, ambaye anatarajiwa kugombea tena urais mwaka huo.

Kupitia akaunti yake rasmi ya mtandao wa X, Muhoozi ameeeleza kuwa Mungu alimwelekeza aelekeze nguvu zake kwenye jeshi ili kuwalinda raia wa Uganda.

“Ningependa kutangaza kuwa sitakuwa kwenye karatasi ya kura mwaka wa 2026. Mwenyezi Mungu aliniambia nijikite kwanza kwenye Jeshi lake. Kwa hivyo, namuunga mkono kabisa Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi ujao”, ameeleza Gen. Muhoozi.

Katika taarifa yake, Muhoozi ameonekana kuweka wazi kuwa ataendelea kutumikia kama Mkuu wa Majeshi akisema kuwa hakuna kitu kitakatifu zaidi hapa duniani kuliko Jeshi la wananchi wa Uganda (UPDF).

“Kwa hiyo, siwezi kufikiria heshima kubwa zaidi kuliko kuwa sehemu ya UPDF. Ni ardhi takatifu!! Mungu ibariki UPDF takatifu na Uganda yenye baraka milele”, alisema Muhoozi.

Rais Yoweri Museveni (80) ambaye anatarajiwa kugombea tena urais mwaka 2026, alichaguliwa tena kwa muhula wa sita mwaka 2021, baada ya kuwa madarakani tangu mwaka 1986.

Licha ya tangazo hili, haijulikani kwa nini Muhoozi alibadili uamuzi wake wa kugombea urais, jambo ambalo limewashangaza mashabiki wake wengi waliokuwa tayari kuanza kampeni za kumuunga mkono.

Mwaka 2023, Muhoozi alitangaza nia yake ya kugombea urais mwaka 2026 akisisitiza kuwa ni wakati wa kizazi kipya kuchukua hatamu za uongozi kwa kuwapumzisha wazee.

“Kwa jina la Yesu Kristo Mungu wangu, kwa jina la vijana wote wa Uganda na dunia, na kwa jina la mapinduzi yetu makubwa, nitasimama kugombea urais mwaka 2026”, ameandika Muhoozi.

Uchaguzi wa mwaka 2026 unatarajiwa kuvutia wagombea mashuhuri kama mwanamuziki aliyegeuka mwanasiasa, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, na Dk. Kizza Besigye, hata hivyo kauli nyingine ya Muhoozi huenda ikabadili mwelekeo wa siasa za Uganda.

Amesema kuwa kamwe vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Uganda havitaruhusu raia kushika madaraka ya Urais pindi baba yake atakapoamua kutokugombea.

“Hakuna raia atakayeongoza Uganda baada ya Rais Museveni. Vikosi vya usalama havitaruhusu hilo. Kiongozi ajaye atakuwa mwanajeshi au polisi”, ameandika.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!