Latest Posts

RC MTAMBI: HATUTAKI FUJO, ZIMECHELEWESHA MAENDELEO MKOANI MARA

 

 

Na Helena Magabe Tarime

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Mtambi, amesema hatavumilia fujo za aina yoyote katika mkoa huo, akibainisha kuwa vurugu zimechelewesha maendeleo ya kiuchumi kwa muda mrefu. Amewatahadharisha wote wanaopanga kufanya fujo au kuvamia mgodi kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi yao.

 

Kauli hiyo aliitoa Aprili 14, 2025, wakati wa hafla ya kukabidhi madawati, viti na meza katika Shule ya Sekondari Ingwe, iliyopo Nyamongo, Wilaya ya Tarime. Katika hafla hiyo, RC Mtambi alikabidhi madawati 310 kwa ajili ya shule ya msingi pamoja na seti ya viti na meza 295 kwa ajili ya shule ya sekondari Ingwe.

 

“Kuna watu wanadhani kuwa mgodi una shea aslimia 100 peke yake wanasahau kuwa Serikali ina ubia wa asilimia na mgodi. Wakiuvamia mgodi, wanavamia pia mali ya Serikali. Uzalishaji wa mgodi huu unawanufaisha Watanzania wote. Mtu yeyote atakayekuja kukwamisha miradi muhimu ya maendeleo, sheria itachukua mkondo wake. Nawaonya pia wanasiasa uchwara na wachochezi wanaotafuta umaarufu kwa kuchochea vurugu — nafasi hiyo haipo,” alisema Kanali Mtambi.

 

Mnamo Februari 26, 2025, katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo, RC Mtambi alitembelea shule moja ya msingi ambapo alikuta wanafunzi wamekalia tofali, ndoo na wengine walileta viti kutoka nyumbani. Tukio hilo lilimghadhabisha, na akaagiza madiwani kutopokea mishahara hadi pale mradi wa madawati utakapotekelezwa.

 

Hatua hiyo ilichochea utekelezaji wa haraka ambapo, Machi 29, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, kwa niaba ya RC Mtambi, alipokea madawati 215 kwa ajili ya Shule ya Msingi Kewanja kutoka kwa mkandarasi RIN Issack Range. Hatimaye, Aprili 14, 2025, madawati ya awamu ya pili yalikabidhiwa rasmi.

 

Meneja wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko, alisema kuwa kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), kampuni hiyo inatekeleza mradi wa kutengeneza madawati 5,765 kwa shule za msingi na seti 3,647 za meza na viti kwa shule za sekondari. Hadi sasa, madawati 890 yamekamilika kwa ushirikiano na wakandarasi wanne.

 

Aliongeza kuwa huo ni utekelezaji wa miradi ya mwaka 2022/2023 inayolenga kutatua changamoto katika kata 26 za Halmashauri ya Tarime Vijijini. Miradi hiyo inajumuisha pia maboresho kwenye sekta za afya, mazingira, barabara na upanuzi wa mradi wa maji Kewanja. Aidha, zaidi ya Shilingi bilioni 4 zimetengwa kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati chini ya kanuni mpya za Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini za mwaka 2024.

Kwa upande wake, Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara, aliushukuru mgodi wa Barrick kwa mchango wake katika maendeleo ya jamii kupitia fedha za CSR, mrahaba wa asilimia 1, na huduma za jamii (service levy). Alisema mgodi huo umeendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo katika mkoa huo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!