Katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika 2025, yaliyoandaliwa na shirika la ActionAid Tanzania katika Kijiji cha Mloda, Kata ya Mlowa Barabarani, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, changamoto za utoro wa wanafunzi na ukatili dhidi ya watoto zimetajwa kuwa sababu kubwa zinazoathiri maendeleo ya elimu na ustawi wa watoto katika mkoa wa Dodoma.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ilikuwa: “Haki za Mtoto: Tulipotoka, Tulipo na Tuendako.”
Watoto Wamekuwa Wafanyakazi, Si Wanafunzi
Afisa Elimu wa Kata ya Mlowa Barabarani, Amani Munna, alieleza kuwa pamoja na jitihada za serikali kutoa elimu bure, watoto wengi hawamalizi shule kwa sababu ya kuingizwa katika shughuli za uzalishaji mali.
“Theruthi moja ya watoto wanaoandikishwa shule wanaacha masomo kabla ya kumaliza darasa la saba. Hii inatokana na baadhi ya wazazi kushindwa kutimiza wajibu wao, hasa kuhakikisha watoto wanapata mahitaji ya msingi shuleni,” alisema Munna.
Aidha, alisisitiza kuwa fursa ya kujiunga na elimu ya Memkwa bado ipo kwa watoto waliokosa nafasi ya kujiunga na mfumo rasmi kwa wakati, hasa wale wenye umri chini ya miaka 10.
Elimu ni Silaha Dhidi ya Ujinga
Munna alionya kuwa jamii isipoandaa watoto wao kwa elimu bora, taifa litazalisha watu wasioweza kujitetea dhidi ya wizi wa rasilimali zao wenyewe.
“Tusipojenga kizazi chenye elimu, tutajikuta tunapoteza rasilimali kwa urahisi kwa sababu ya ujinga wa kizazi chetu,” alionya.
Wazazi Watafuteni Riziki, Lakini Msisahau Malezi
Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Chamwino, Maua Katengu, aliwataka wazazi kubeba jukumu la malezi kwa vitendo – si kwa mapenzi tu, bali kwa onyo, maelekezo na nidhamu.
“Tuwapende watoto kwa maana halisi; kuwapenda ni pamoja na kuwaonya na kuwaelekeza. Tusilea watoto kama mayai – tusitengeneze kizazi chenye shida,” alisema.
Aidha, alionya juu ya maudhui yasiyofaa ambayo watoto wanakutana nayo kwenye mitandao ya kijamii, televisheni, na vibanda vya sinema, akisema mengi hayaendi sambamba na maadili ya kijamii.
Tuwasikilize Watoto Wetu
Katengu aliwasihi wazazi kuwa karibu na watoto wao, kuzungumza nao mara kwa mara ili kujua changamoto zinazowakabili.
“Inasikitisha mzazi kuwa wa mwisho kujua mtoto wake amefanyiwa ukatili wakati majirani wote wanajua. Tuwe na mazoea ya kula nao pamoja, kutoka nao pamoja, ili wawe na nafasi ya kutufikia,” alisema kwa msisitizo.
Ukatili Unaanzia Nyumbani
Afisa Maendeleo ya Kata ya Mlowa Barabarani, Christina Gambo, alisema ukatili mwingi dhidi ya watoto unatokea mikononi mwa watu wa karibu, hasa nyumbani.
“Watoto wanabakwa, wanapigwa, wanadhalilishwa na watu tunaowaamini kama wasaidizi wa nyumbani. Halafu sisi wazazi tunawanyamazisha badala ya kuripoti – huu ni mkosaji wa haki za mtoto,” alisema.
Burudani, Ujumbe wa Maadili
Maadhimisho hayo yalipambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa watoto, ikiwa ni pamoja na:
- Mpira wa miguu na netiboli,
- Ngoma za asili,
- Ngonjera na mashairi,
- Maigizo yenye ujumbe wa kuelimisha jamii kuhusu ukatili na umuhimu wa haki za mtoto.
Historia ya Siku ya Mtoto wa Afrika
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika hufanyika kila Juni 16, yakiwa ni kumbukumbu ya maandamano ya watoto wa Soweto, Afrika Kusini mwaka 1976 waliodai haki ya kupata elimu bora na kupinga ubaguzi wa rangi. Siku hii huangazia haki na ustawi wa mtoto kama yalivyobainishwa kwenye Ibara ya 2 hadi 22 ya Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto.