Latest Posts

BOBI WINE HAKUPIGWA RISASI, ALIJIKWAA: POLISI UGANDA WAELEZA HUKU BOBI AKITARAJIWA KUFANYIWA UPASUAJI

Na Amani Hamisi Mjege.

Polisi nchini Uganda imesema kuwa kiongozi wa chama cha Jukwaa la Umoja wa Kitaifa (NUP) Robert Kyagulanyi Ssentamu alijikwaa wakati akiingia kwenye gari lake na kusababisha jeraha la mguu wake, wakati ambao “Kyagulanyi na timu yake wanadai kwamba alipigwa risasi”.

Kwa mujibu wa msemaji wa Polisi Rusoke Kituuma, tarehe 3 Septemba 2024, Kyagulanyi Robert alialikwa na Wakili George Musisi kwenye sherehe ya shukrani huko Bulindo ambayo ilimalizika kwa amani, hata hivyo Kyagulanyi pamoja na timu yake waliposhuka kutoka kwenye magari yao na walianza kuandamana.

“Polisi walipendekeza kwamba wasifanye hivyo. Licha ya maelekezo yao, Mheshimiwa Kyagulanyi alisisitiza kuendelea na maandamano hayo na kufunga barabara, jambo ambalo lililazimisha polisi kuingilia kati ili kuzuia maandamano”, ilieleza taarifa ya polisi.

Polisi wamesema watafanya uchunguzi ili kubainisha ukweli wa tukio hilo la kudaiwa kupigwa risasi na matukio yoyote yanayohusiana.

Wakati taarifa ya jeshi la polisi ikieleza kuhusu kujikwaa kwa Bobi Wine, chama chake cha NUP kupitia kwa msemaji wake Joel Ssenyonyi kimesema kwamba baada ya Bobi Wine kuondoka kutoka sherehe ya mwanasheria, umati wa watu ulijikusanya na polisi walianza kurusha gesi ya machozi na miripuko mingine.

“Kipande cha gesi ya machozi kilipigwa kwenye mguu wa kushoto wa Mheshimiwa Bobi Wine, na kusababisha jeraha kubwa… Polisi wamechapisha taarifa wakisema kwamba Mheshimiwa Bobi Wine aliteleza na kuanguka alipokuwa akiingia kwenye gari lake, na hivyo kupata jeraha hilo, jambo ambalo ni dhihaka!”, alieleza Joel.

Bobi Wine atafanyiwa upasuaji kutokana na jeraha alilolipata. Wakili wa mwanasiasa huyo, George Musisi ameufahamisha umma siku ya Jumatano kwamba hivi sasa hayuko katika hali mbaya ingawa kwa mujibu wa madaktari atafanyiwa upasuaji kuondoa vipande vya bomu la kutoa machozi lililompiga mguuni.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!