
Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) imetakiwa kuhamasisha wawekezaji kuwekeza katika kongani ya viwanda inayojengwa kijiji cha Maranje Halmashauri ya Mji Nanyamba Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara.
Hayo ameyaeleza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo DK.Hussein Mohamed alipotembelea kongani hiyo ya viwanda kwenye eneo hilo la Maranje mkoani Mtwara,amesema serikali pekee haiwezi kuendelesha kongani hiyo hivyo wanahitaji uwekezaji kutoka sekta binafsi ambao wako tayari.
‘’Lengo la serikali ifikapo mwaka 2030 asilimia 100 ya korosho inayozalishwa yote ibanguliwe nchini, maana yake ni lazima tuwe na viwanda vya kutosha vya kubangua nchini na hii siyo pake yake na ufuta pia kwahiyo lazima tuwe na hivi viwanda vya kuongeza thamani.’’Amesema Hussein.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa CBT, Mangile Malegesi amesema eneo lote hilo la kongani lina jumla ya hekari 1,572 linalotarajiwa kuwa viwanda zaidi ya 60 na magahala zaidi ya 100 yenye uwezo wa kuhifadhi tani elfu 10,000 ambapo yanatarajiwa kukamilika ifikapo Mei 30,2025.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo utakwenda kusaidia mkoa wa Mtwara na Kanda nzima ya Kusini kuchangamka na kutoa fursa nyingi za ajira kutoka kwenye eneo hilo la Maranje hadi kwa mikoa mingine hususani kwa wanawake na vijana.
Pia amezitaja faida mbalimbali zitazotokana na kongani hiyo ikiwemo ajira za kawaida takribani 35 elfu kwa watu watapata ajira za moja kwa moja, uuzaji wa korosho na bidhaa zake badala ya kuuza tu korosho ghafi kama vile ganda lenyewe.
Sambamba na hilo Naibu Katibu Mkuu huyo, ametembelea Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Nchini (TARI) Naliendele na akiwa katika taasisi hiyo amesema hadi kufikia mwaka 2050 nchi iweze kufikia uchumi wa kati wa juu na ili kufikia hapo moja ya sekta ya mageuzi ikiwemo sekta ya kilimo.
Mkuu wa wilaya ya Mtwara Abdallah Mwaipaya ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia wakulima pembejeo jambo lililochochea kuongeza zaidi uzalishaji wa zao la korosho ikiwa ni pamoja na bei nzuri ambayo haijawahi kutokea.