Mahakama ya mwanzo Morogoro kituo cha Ngerengere imetaja kesi kwa mara ya kwanza ya namba 46 ya mwaka 2025 shtaka la shambulio la kawaida kifungu namba 240 inayomhusu mwalimu wa shule ya msingi Nyambogo aliyefahamika kwa jina la Marry Wilbroad (38) kupigwa na mzazi wa mwanafunzi aliyefahamika kwa jina la Hamisi Kashasha.
Akisoma kesi hiyo Hakimu Mkuu wa Mahakama ya mwanzo kituo cha Ngerengere Venance Mwamunyange amesema shauri hilo limetajwa Machi 10,2025 na litasikilizwa tena Machi 20,2025 huku mzazi huyo akikabiliwa na mashtaka mawili shambulio la kawaida kifungu namba 240 kanuni ya adhabu sura ya 16 na shtaka la pili ni kufanya fujo kifungu namba 87 kanuni ya adhabu sura ya 16.
Tukio hilo la kushambuliwa kwa mwalimu huyo anayefundisha darasa la awali shule hiyo ya Nyambogo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro lilitokea Machi 3 2025 baada ya mwalimu huyo kumparua mwanafunzi kwenye kiwiko cha mkono wakati akiwatoa wanafunzi waliojificha darasani kipindi cha kufanya usafi ndipo mtoto huyo alikimbia kwenda nyumbani kwa mzazi wake na baadae mzazi huyo alikuja eneo la shule na kumshambulika mwalimu huyo kwa kumpiga makofi maeneo ya shingo na shavu.