Latest Posts

CWT IMEWAACHA NETO, TUNAHITAJI MWENYEKITI JASIRI: MGOMBEA MBEYA DC

 

Na Josea Sinkala, Mbeya.

Chama cha walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya kinatarajia kufanya uchaguzi wa viongozi mbalimbali ijumaa ya Machi 21, 2025.

Wagombea wasiopungua watano wamejitokeza kuomba nafasi ya mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Mbeya ambapo nafasi zitakazochaguliwa ni mwenyekiti wa wilaya, mweka hazina na wajumbe wawili kutoka kwenye kila kundi la walimu wa shule za msingi, upili, kundi la wanawake na lile la vijana.

Akizungumza kuelekea uchaguzi huo, mgombea mmoja wapo wa nafasi ya mwenyekiti wa CWT mwalimu Wiliam Msokwa amesema chama cha walimu kinahitaji kiongozi jasiri na mwenye kubeba vilio vya walimu ikiwemo kiwango kikubwa cha makato ya asilimia mbili ya mishahara ikiwezekana ipunguzwe kuwa asilimia moja pamoja na marekebisho ya vipengele mbalimbali vya katiba ya chama hicho cha kitaaluma ikiwemo kuweka ukomo wa madaraka tofauti na ilivyo sasa.

Pia ameeleza suala la kikokotoo kuwa bado ni mwiba kwani walimu wanataka kikokotoo kama ilivyokuwa awali tofauti na kikokotoo cha sasa akisema wastaafu wanatakiwa kupata malipo yao kwa mkupuo.

Alipoulizwa kuhusu sakata la walimu wasio na ajira (NETO), mwalimu Wiliam Msokwa amesema walimu hao wamebaki kama yatima kwani CWT ilikuwa na wajibu wa kuungana na wadau wengine kuwapigia kelele ikizingatiwa pia kwamba kada ya ualimu haijajitosheleza kwani ina walimu wasiojitosheleza.

Amesema CWT kuanzia ngazi ya wilaya hadi Taifa inahitaji viongozi bora na wenye kutetea haki na maslahi ya walimu ili kurejesha nguvu na matumaini ya walimu kama ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita ambapo Chama cha walimu Tanzania kilikuwa sauti ya walimu juu ya shida zinazowakabili.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!