Latest Posts

MIRADI YA MAENDELEO YANYAKUA BILIONI 500 SIMIYU

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringi Macha, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetoa zaidi ya shilingi bilioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo, hususan katika sekta za elimu, barabara, nishati na reli.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Julai 18,2025  jijini Dodoma, wakati akieeleza Mafanikio ya serikali ya awamu ya sita Rc Macha ameeleza  kuwa kati ya mwaka 2020 hadi 2025, Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 119.9 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu katika mkoa wa Simiyu.

“Katika kipindi hiki, fedha hizo zimetumika kujenga na kukamilisha miundombinu ya shule za msingi, sekondari na vyuo. Hatua hii imeongeza upatikanaji wa elimu kwa wanafunzi wa ngazi mbalimbali,” amesema  Macha.

Ameongeza  kuwa bajeti ya elimu bila ada kwa shule za msingi na sekondari imeongezeka kutoka shilingi bilioni 6.81 mwaka 2020 hadi shilingi bilioni 37.7 mwaka 2025. Aidha, idadi ya shule za msingi imeongezeka kutoka 513 hadi 611, na shule za sekondari kutoka 167 hadi 197 katika kipindi hicho.

Miongoni mwa shule mpya zilizojengwa ni Shule ya Sekondari ya Bweni ya Wasichana ya Mkoa wa Simiyu, ambayo imejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 4.5 na kuzinduliwa rasmi na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika sekta ya miundombinu ya barabara, Macha amesema  kuwa Mkoa wa Simiyu umepokea jumla ya shilingi bilioni 257.5 kwa ajili ya uboreshaji wa barabara, ambapo shilingi bilioni 70.4 zimetumika katika miradi inayosimamiwa na TARURA, na shilingi bilioni 187.1 katika miradi ya TANROADS.

Kuhusu ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, Macha ameeleza  kuwa kipande cha tano cha reli hiyo chenye urefu wa kilomita 341 kinapita mkoani Simiyu. Ujenzi wake ulianza tarehe 15 Mei 2021 kwa gharama ya shilingi trilioni 3.

“Kukamilika kwa reli hii kutasaidia kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo, bidhaa na abiria, sambamba na kupunguza uharibifu wa barabara,” ameeleza .

Kwa upande wa nishati, Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 130.8 kati ya mwaka 2020 hadi 2025 kwa ajili ya usambazaji wa huduma ya umeme mkoani humo. Pia, ujenzi wa kituo kikubwa cha kupoza umeme unaendelea kwa gharama ya shilingi bilioni 49.

Macha amebainisha kuwa lengo la Serikali ni kuunganisha umeme katika kaya 231,850 kati ya 317,000 ifikapo mwaka 2030 kupitia Mpango wa Taifa wa Upatikanaji wa Nishati (National Energy Compact).

Macha amehitimisha  kwa kusema kuwa mafanikio hayo ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kwa usawa katika mikoa yote, ikiwemo ile ya pembezoni kama Simiyu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!