Latest Posts

WASIRA: UCHAGUZI UTAAHIRISHWA TU KAMA KUNA VITA, NA VITA HAIPO

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amesema kuwa kauli ya baadhi ya vyama vya siasa na wanaharakati wanaodai kwamba uchaguzi mkuu ujao uahirishwe hadi mchakato wa marekebisho ya mfumo wa uchaguzi utakapotekelezwa, haina mashiko wa kisheria wala wa kisera.

Akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kilichorushwa na ITV, Wasira amesema ingawa anaheshimu hoja hiyo kwa upande wa walioileta, yeye binafsi haioni kama ina msingi wowote wa kimantiki na kikatiba.

“Kwangu mimi hoja ya ‘No Reforms, No Election’ haina mashiko. Lakini sisemi kwa wale wanaoisema haina mashiko; labda kwao ina mashiko, ila mimi sio msemaji wao. Sijaelewa wanataka tufanye reforms gani zaidi baada ya tuliyokwisha kufanya,” amesema Wasira.

Amefafanua kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uchaguzi mkuu hauwezi kuahirishwa kwa sababu yoyote ile isipokuwa tu katika hali ya vita.

“Wanasema tuahirishe uchaguzi. Haiwezekani. Uchaguzi ni jambo kubwa. Katiba inasema wazi kuwa hatuwezi kuahirisha uchaguzi isipokuwa kuwe na vita, na vita haipo. Mashiko yapo wapi sasa?” amehoji.

Kwa mujibu wa Wasira, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imekwishatekeleza hatua nyingi za marekebisho ya mfumo wa uchaguzi na kisiasa kwa mujibu wa mapendekezo ya wadau.

“Tumeshaeleza kwenye Ilani kuwa tutazungumza kuhusu Katiba mpya baada ya uchaguzi. Hii si kauli ya CCM tu, bali ni mapendekezo ya kikosi kazi kilichoshirikisha vyama vyote isipokuwa Chadema,” amesema.

Akijibu swali kuhusu hali ya siasa nchini na hisia za baadhi ya wananchi kuwa kuna mazingira ya ukandamizaji au kutoridhika, Wasira amesema kuwa ni jambo la kawaida kwa watu kunung’unika hata pale ambapo hali ni nzuri. “Hakuna nchi duniani isiyo na watu wanaonung’unika. Hakuna. Hata ufanye nini, kutakuwa na mtu pale anayeumwa au ana tatizo lake,” amesema.

Akimkumbuka Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Wasira alisema aliwahi kumweleza kuwa nchi haiwezi kuwa kimya kama ugali wa jana. “Nchi lazima iongee, lazima kuwe na mijadala, migongano ya mawazo. Hiyo ndiyo afya ya taifa. Kama hakuna anayeongea, Rais atajuaje kuna tatizo na tatizo lipo wapi?” amesema.

Hata hivyo, Wasira amesema kwa tathmini yake, hali ya kisiasa na kijamii nchini ni nzuri, licha ya uwepo wa changamoto. “Siwezi kusema Tanzania haina matatizo. Nikikwambia hakuna matatizo, utakuwa na haki ya kunipeleka hospitali ya afya ya akili. Matatizo yapo, watu wananung’unika, lakini nchi iko salama na mambo yanaendelea vizuri,” amesisitiza.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!