Ukusanyaji wa mapato ni moja ya ajenda za kudumu katika vikao vya Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita. Katika mwaka wa fedha 2024/2025, Halmashauri hiyo ilivuka lengo la ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 125.19, ambapo jumla ya Shilingi bilioni 10.4 zilikusanywa. Hii ni sawa na ongezeko la Shilingi bilioni 2.1 kutoka bajeti iliyokadiriwa ya Shilingi bilioni 8.3.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ndg. Karia Rajab Magaro, amekuwa akisisitiza kwa watendaji wote kuwa waadilifu katika ukusanyaji wa mapato, huku akiwataka kuwa wabunifu katika kusimamia na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ndani ya Halmashauri.
Kupitia usimamizi mzuri wa mapato ya ndani, miradi mbalimbali imetekelezwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo jumla ya Shilingi bilioni 3.1 zilitengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule, zahanati, vituo vya afya, nyumba za watumishi na ofisi za kata.
Aidha, kupitia mapato ya ndani pamoja na fedha za marejesho, Halmashauri imeweza kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Jumla ya Shilingi bilioni 1.8 imetolewa kwa wananchi waliokidhi vigezo vya kupata mikopo hiyo.
Ili kuhakikisha kuwa huduma bora zinaendelea kutolewa kwa wananchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali kama shule, zahanati, vituo vya afya na miundombinu ya barabara, Halmashauri ya Wilaya ya Geita inaendelea na mipango ya kutwaa maeneo ya uwekezaji ili kuongeza vyanzo vya mapato.
Mnamo Julai 24, 2025, Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi, CPA Eveline Ntahamba, ilifanya ziara katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro kwa ajili ya kukagua maeneo ya uwekezaji. Timu hiyo ilitembelea eneo lenye ukubwa wa hekari 14 ambalo Halmashauri inatarajia kulitwaa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha mabasi cha Katoro (Katoro Bus Stand), pamoja na eneo la Soko la Kariakoo Katoro, ili kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika soko hilo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita inaendelea kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna inavyotoa fedha nyingi kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.