Latest Posts

TUME HURU YA TAIFA YA UCHAGUZI YAHIMIZA USHIRIKI WA WATU WENYE ULEMAVU KATIKA UCHAGUZI MKUU 2025

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufani) Jacob Mwambegele, leo Alhamisi Julai 31, 2025 ameongoza mkutano muhimu kati ya Tume na Wawakilishi wa Watu Wenye Ulemavu uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, kuhusu maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Akizungumza kwa niaba ya Tume, Jaji Mwambegele amewashukuru na kuwapongeza wawakilishi hao kwa kuitikia wito na kushiriki kwenye mkutano huo ambao ni sehemu ya mikutano ya wadau wa uchaguzi inayoendelea kufanyika kuanzia tarehe 27 Julai hadi 3 Agosti, 2025.

“Tume inatambua kuwa watu wenye ulemavu ni wadau muhimu wa uchaguzi na hivyo ina wajibu wa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika mchakato huu,” alisema Jaji Mwambegele huku akisisitiza kuwa kikao hicho ni fursa ya kubadilishana mawazo, kutoa hoja, kueleza changamoto na kutafuta njia za kuzitatua kwa pamoja.

Katika hotuba yake, Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa Tume ilitangaza rasmi ratiba ya Uchaguzi Mkuu tarehe 26 Julai, 2025. Utoaji wa fomu kwa wagombea wa Urais na Makamu wa Rais utaanza tarehe 09 hadi 27 Agosti, huku fomu za Ubunge na Udiwani zikitolewa kuanzia tarehe 14 hadi 27 Agosti. Uteuzi wa wagombea wote utafanyika tarehe 27 Agosti, 2025 ambapo kampeni zitaanza rasmi tarehe 28 Agosti na kumalizika tarehe 28 Oktoba kwa Tanzania Bara na 27 Oktoba kwa upande wa Zanzibar.

Jaji Mwambegele amebainisha kuwa mwaka 2024 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria mbili muhimu za uchaguzi ambazo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024. Kufuatia sheria hizo, Tume imetunga Kanuni za Uchaguzi, Kanuni za Maadili na kutoa Maelekezo kwa wadau wa uchaguzi, watendaji na waangalizi.

Ameongeza kwa kusema kuwa, Tume imetangaza kuwa jumla ya majimbo 272 yatatumika katika uchaguzi wa mwaka huu, yakiwemo majimbo 8 mapya Tanzania Bara. Aidha, kata 3,960 zitahusika na uchaguzi wa madiwani, ambapo kata 4 ni mpya zilizoongezwa baada ya kuanzishwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI.

Mwenyekiti huyo pia ameipongeza jamii ya watu wenye ulemavu kwa mchango wao mkubwa katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililofanyika kuanzia tarehe 20 Julai, 2024 hadi tarehe 04 Julai, 2025.

Katika kuhakikisha uwazi, Tume imekuwa ikiendesha mikutano na wadau mbalimbali wa uchaguzi, ambapo mkutano huo na watu wenye ulemavu ni sehemu ya utekelezaji wa azma hiyo.

Kuhusu elimu ya mpiga kura, Jaji Mwambegele amesema Tume imejipanga kutumia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, mikutano, maonesho, machapisho na magari ya matangazo katika kuifikisha elimu hiyo kwa umma.

Aidha, taasisi 164 zimepewa vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura wakati huu wa uchaguzi, huku taasisi 88 (76 za ndani na 12 za kimataifa) zikiwa zimepata vibali vya kuangalia uchaguzi huo.

Katika hatua nyingine, Tume imeandaa karatasi za kura zenye maandishi ya nukta nundu kwa ajili ya watu wasioona, sambamba na maandalizi ya vituturi vinavyoweza kubadilishwa ili kuwapa fursa ya kupiga kura kwa faragha watu wenye ulemavu wa viungo.

Jaji Mwambegele amesisitiza kuwa Tume itaendelea kuwashirikisha watu wenye ulemavu na wadau wote katika kila hatua ya uchaguzi, na kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa huru, wa haki, wa wazi na unaoaminika kwa kila Mtanzania.

Kwa kauli mbiu ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 isemayo “KURA YAKO HAKI YAKO – JITOKEZE KUPIGA KURA” ambapo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imehimiza kila mmoja kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kidemokrasia wa Taifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!