Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amefanya ukaguzi wa mwanzo wa ujenzi wa barabara ya Mbagala Rangitatu hadi Kongowe, mradi unaotarajiwa kuboresha usafirishaji miongoni mwa wananchi wa Dar es Salaam, Pwani na mikoa ya Kusini.
Barabara hii yenye urefu wa kilometa 3.8 itakuwa na njia nne, ikiwa ni pamoja na njia katikati kwa ajili ya Mabasi Yaendayo Haraka, na njia pembeni kwa usafiri wa kawaida. Mradi unatekelezwa na kampuni ya STECOL Corporation kwa gharama ya Shilingi bilioni 54.5, na ujenzi unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 15, mwishoni mwa Novemba 2026.
Akizungumza baada ya ukaguzi, Mhandisi Besta amesema:
“Tumefanya kikao na mkandarasi na ametuhakikishia kuanza haraka kuleta vifaa na wataalamu (mobilization) ili kazi ziende kwa kasi ili kuondoa changamoto ya msongamano iliyopo. Barabara hii ni muhimu sana kwa wananchi wanaosafiri kuelekea mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara”
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Alinanuswe Kyamba, amesema timu yao imejipanga kumsimamia mkandarasi kuhakikisha kwamba anatimiza kazi ipasavyo kwa viwango vinavyohitajika na kwa muda uliopangwa.
Barabara ya Mbagala Rangitatu hadi Kongowe ni sehemu ya mradi mkubwa wa miundombinu unaolenga kuongeza ubunifu wa biashara na maendeleo ya viwanda kutoka Dar es Salaam hadi Mtwara, huku ikiboresha usafirishaji wa bidhaa za viwandani na kupunguza foleni kwenye barabara kuu