Mtendaji Mkuu ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, Septemba 19, 2025 amefanya ukaguzi wa kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Kwanza, package A, unaotoka Ubungo hadi Kimara jijini Dar es Salaam, ambapo ametoa maelekezo ya kuongeza kasi ya kazi ili mradi ukamilike kwa wakati.
Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 83.8 unafadhiliwa na Benki ya Dunia, na hadi sasa umekamilika kwa takribani asilimia 60.
Hii ni hatua kubwa ikilinganishwa na miezi tisa iliyopita ambapo utekelezaji wake ulikuwa umefikia asilimia 21 pekee.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mhandisi Besta amesema, upanuzi wa barabara kutoka njia nne hadi sita ni hatua muhimu itakayosaidia kupunguza foleni kwa kiasi kikubwa.
“Miradi yote ya BRT kuanzia Awamu ya Kwanza hadi ya Nne (Lot 1 na 2) inaendelea jijini Dar es Salaam, na TANROADS itaendelea kusimamia ubora wa ujenzi ili kupunguza msongamano wa magari,” alisema.
Ameongeza kuwa kutokana na mvua zinazotarajiwa kunyesha, wakandarasi wamelazimika kuongeza kasi ya kazi.
“Ni lazima tuongeze nguvu ili mradi ukamilike kwa wakati na kutoa nafuu ya usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa BRT, Mhandisi Allen Natai, amesema mkandarasi anaendelea na utekelezaji na kushauriwa kuendelea kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa.
Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Alinanuswe Kyamba, amesema wamepokea maelekezo ya Mtendaji Mkuu na watahakikisha wanayatekeleza kwa vitendo ili kumsukuma mkandarasi kumaliza kazi kabla ya mvua kuanza kunyesha