Latest Posts

MWENEZI CCM MTWARA: DKT. SAMIA ATANADI SERA ZAKE MTWARA SEPTEMBA 23

Ikiwa tayari amezunguka katika mikoa mbalimbali akinadi sera zake kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwasili mkoani Mtwara Septemba 23, 2025 kwa ajili ya kuendelea na kampeni.

Akizungumza na vyombo vya habari, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Mtwara Juma Namkoveka, amesema kupitia ziara hiyo Rais Samia atakutana na wananchi kupitia mikutano ya kampeni kwa lengo la kuwaeleza dira, sera na mikakati ya chama kwa maendeleo ya Taifa kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025–2030.

Amesema pia Rais atazungumzia mafanikio mbalimbali yaliyopatikana chini ya Serikali ya Awamu ya Sita hususani utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika kipindi chake hivyo amewaomba wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika mikutano hiyo ili kumsikiliza Rais na Mgombea Urais wao.

Namkoveka amesisitiza wananchi kuendelea kudumisha amani, mshikamano na mshirikiano wakati wote wa ziara hiyo ili kuonyesha umoja wa wananchi wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla.

Rais Samia anatarajiwa kuwasili wilayani Nanyumbu akitokea mkoani Ruvuma, ambapo atafanya mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Kituo Kikuu cha Mabasi na mkutano mwingine utafanyika katika Uwanja wa Boma wilayani Masasi.

Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Mtwara wamesema wanamsubiri kwa hamu ujio wa mgombea huyo, ili wapate kusikiliza sera zake huku matarajio yao makubwa yakiwa ni kuona mabadiliko zaidi katika sekta za huduma za kijamii.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!