Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema uundwaji wa Tume Huru ya Kufanya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 umezingatia matakwa ya Sheria ambayo inampa mamlaka ya kuunda tume maalum kuchunguza masuala nyeti ya kitaifa.
Akizungumza Ikulu Chamwino, Dodoma, Novemba 20, 2025 wakati wa uzinduzi wa tume hiyo, Rais Samia amesema lengo la kwanza ni kuhakikisha Tanzania inafanya uchunguzi wa ndani kabla ya kuhusisha tume kutoka nje ya nchi.
“Niliona kabla ya kuletewa tume za nje, tuwe na tume yetu ya ndani ifanye kazi. Na za nje zikija zitakuja kuzungumza na tume mwenzao ambao tayari wameshaanza hiyo kazi,” amesema.
Amesema tukio lililotokea halikutarajiwa kwa nchi yenye historia ndefu ya amani, utulivu na ustahimilivu wa kisiasa kama Tanzania.
Katika maelekezo yake, Rais Samia ameitaka tume hiyo kuchunguza maeneo makuu kadhaa ikiwamo kiini cha vurugu na sababu za kuzuka kwa kadhia, madai ya vijana waliotoka barabarani na kauli za vyama vya upinzani.
Aidha amesema kuwa kazi ya Tume hiyo ndiyo itakayoweka msingi wa ajenda na dira ya Tume ya Maridhiano aliyoiahidi kuunda ndani ya siku 100 tangu awe Rais.
Amesema tume imepewa dhamana kubwa ya kutazama kwa undani hatua zote zilizochukuliwa kabla, wakati na baada ya vurugu, ili nchi iweze kupata majibu ya msingi kabla ya kuanza safari ya maridhiano ya kitaifa.
“Wakati nazindua kampeni niliahidi kwamba ndani ya siku 100 nitaweka tume ya maridhiano… Lakini kwa hili lililotokea tumeona tuunde tume hii kwanza ifanye kazi yake imalize. Mapendekezo yatakayotoka huku ndiyo tutakayokwenda kuyafanyia kazi kwenye tume ile ya maridhiano.” Ameeleza.
Akiweka wazi matarajio ya muda wa utekelezaji, amesema kazi ya awali inatarajiwa kufanyika kwa miezi mitatu, ingawa muda unaweza kurekebishwa kulingana na mwenendo wa uchunguzi.