Dunia imeshtushwa na taarifa za kuuawa kwa Saif al-Islam Gaddafi (53), mwana wa kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi, ambaye kwa muda mrefu alionekana kama mrithi wa kiti cha enzi cha baba yake.
Tukio hilo limetokea Jumanne, Februari 3, 2026, ambapo watu wanne wenye silaha wasiojulikana walivamia nyumba yake katika mji wa Zintan, kaskazini magharibi mwa Libya. Waendesha mashtaka nchini humo wamethibitisha kuwa Saif al-Islam alifariki kutokana na majeraha ya risasi baada ya “makabiliano ya moja kwa moja” na wavamizi hao.
Serikali ya Urusi, kupitia msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Maria Zakharova, imelaani vikali mauaji hayo ikiyataja kuwa ni “uhalifu mkubwa.” Urusi, ambayo imekuwa na uhusiano wa karibu na Saif al-Islam, imetoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kina na wa haraka ili kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wahusika.
Licha ya maelezo ya waendesha mashtaka na wakili wake (kupitia shirika la AFP) kusema shambulio lilitokea Zintan, dada yake Saif al-Islam ametoa kauli tofauti kupitia televisheni ya Libya akidai kuwa kaka yake alifariki karibu na mpaka wa nchi hiyo na Algeria.
Saif al-Islam alikuwa akitazamwa kama kiongozi mwenye ushawishi ambaye angeweza kuirejesha familia ya Gaddafi madarakani. Mnamo mwaka 2021, mamlaka nchini Libya zilitoa waranti ya kumkamata kwa tuhuma za kuwa na uhusiano na kundi la mamluki la Urusi, Wagner, ambalo sasa limevunjwa na nafasi yake kuchukuliwa na kikosi cha Africa Corps kinachofadhiliwa na serikali ya Urusi.
Hadi sasa, haijafahamika ni nani aliyekuwa nyuma ya kikosi hicho cha “makomandoo wanne” kilichotekeleza mauaji hayo, huku wataalamu wa uchunguzi wa jinai wakipelekwa Zintan kuanza kazi ya kusaka ukweli.