Nyaraka mpya zilizowekwa wazi hivi karibuni kuhusu mfanyabiashara na mhalifu wa makosa ya kingono wa Marekani, marehemu Jeffrey Epstein, zimeibua madai ya kuwepo kwa uhusiano wa kifedha kati yake na aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, marehemu Robert Mugabe.
Kwa mujibu wa nyaraka hizo, mawasiliano ya barua pepe ya mwaka 2015 kati ya Epstein na mjasiriamali wa Kijapani, Joi Ito, yanaonesha kuwa Epstein alipendekeza mpango wa kukutana na Rais Mugabe. Lengo la mpango huo lilikuwa ni kuanzisha sarafu mpya nchini Zimbabwe kufuatia kuporomoka kwa dola ya nchi hiyo kutokana na mfumuko wa bei uliokithiri.
Nyaraka za Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) za mwaka 2017 zimeongeza uzito wa madai hayo kupitia “chanzo cha siri.” Chanzo hicho kilidai kuwa Epstein alikuwa akifanya kazi kama meneja wa utajiri wa viongozi wenye ushawishi mkubwa duniani, akiwemo Rais wa Urusi Vladimir Putin na Robert Mugabe.
Hata hivyo, hadi sasa, madai hayo bado hayajathibitishwa na vyanzo vingine huru na sheria inabainisha kuwa kutajwa kwenye faili za Epstein si uthibitisho wa kisheria wa kufanya makosa au kushiriki katika uhalifu.
Robert Mugabe alifariki mnamo Septemba 2019 akiwa na umri wa miaka 95, huku Jeffrey Epstein akikutwa mfu gerezani mwezi mmoja kabla (Agosti 2019) akisubiri kesi ya biashara haramu ya ngono.
Kulingana na BBC, hakuna tamko rasmi kutoka upande wa familia ya kiongozi huyo aliyetawala Zimbabwe kwa miongo kadhaa tangu uhuru.