Latest Posts

MAREKANI YAISHUTUMU CHINA KUFANYA MAJARIBIO YA SIRI YA NYUKLIA; TRUMP ATAKA MKATABA MPYA NA WA KISASA.

Marekani imetoa wito wa dharura wa kufanyika kwa mazungumzo ya pande tatu kati yake, Urusi, na China ili kuweka mipaka mipya ya silaha za nyuklia, huku ikiishutumu Beijing kwa kufanya majaribio ya siri ya silaha hizo hatari.

Wito huo umekuja Februari 6, 2026, siku moja baada ya kumalizika kwa mkataba wa New START- makubaliano ya mwisho yaliyokuwa yanadhibiti nguvu za nyuklia kati ya Washington na Moscow. Kumalizika kwa mkataba huo kumeacha dunia bila sheria yoyote ya kuzuia mlimbikizo wa silaha zinazoweza kuteketeza sayari, jambo linalozua hofu ya kurejea kwa kasi kwa mashindano ya silaha (Arms Race).

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio kupitia andiko lake la mtandao amesisitiza kuwa udhibiti wa silaha hauwezi tena kuwa suala la nchi mbili tu. Marekani inadai kuwa China inatumia mwanya wa kutofungwa na mkataba wowote kupanua ghala lake la nyuklia kwa kasi ya kihistoria.

Marekani inakadiria China itakuwa na zaidi ya vichwa vya nyuklia 1,000 kufikia mwaka 2030. Aidha Washington imeituhumu Beijing kufanya majaribio ya milipuko ya nyuklia kwa siri, ikiwemo ule wa Juni 22, 2020, kinyume na ahadi za kimataifa.

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, alipendekeza kuongezwa kwa mkataba wa New START kwa mwaka mmoja, lakini Rais Donald Trump alikataa na kusema anataka mkataba “mpya na wa kisasa.” Urusi sasa inapendekeza kuwa mazungumzo yoyote yajumuishe pia Uingereza na Ufaransa. Hata hivyo, Uingereza imegoma ikidai kuwa msisitizo uwe kwa nchi zenye maghala makubwa Zaidi- Marekani, Urusi, na China.

Balozi wa China nchini Uswisi, Shen Jian, amezipuuza shutuma za Marekani akiziita ni “kauli zisizo na uwajibikaji.” Beijing imesisitiza kuwa haina mpango wa kujiunga na mazungumzo ya upunguzaji silaha katika hatua hii, ikidai kuwa wenye maghala makubwa zaidi (Marekani na Urusi) ndio wenye jukumu la kwanza.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!