
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), imeanza ujenzi wa vituo maalumu vya mafunzo ya ufundi kwa vijana waliokosa elimu ya msingi (IPOSA) katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Tabora, Kigoma na Songwe.
Ujenzi wa vituo hivyo ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata haki ya elimu bora na yenye usawa, bila kujali changamoto za kimazingira.
Akizungumza wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho katika Shule ya Msingi Kaliua mkoani Tabora Msimamizi wa Miradi ya IPOSA kutoka TEA Bw. John Mtiba amesema, mradi unaendelea vizuri ambapo ujenzi umefikia asilimia 97.
Ameeleza kuwa ana imani mradi utakamilika kwa wakati na kuanza kutumika ili kuwasaidia vijana kupata ujuzi katika fani mbalimbali, jambo litakalowawezesha kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.
Aidha, Bw. Mtiba ameongeza kuwa miradi hiyo inafadhiliwa na UNICEF kwa kushirikiana na TEA, na inatarajiwa kugharimu takribani shilingi bilioni 1. Miradi hii itakapokamilika itawawezesha zaidi ya vijana 800 wa kike na wa kiume kupata ujuzi wa ufundi katika fani mbalimbali kwenye kila kituo.