Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amefichua siri ya mazungumzo yake na Rais wa Marekani, Donald Trump, akibainisha kuwa mashambulizi makali dhidi ya miundombinu ya Iran na Lebanon sasa yanatumiwa kama nguvu ya kulazimisha makubaliano yatakayomaliza vita kwa faida ya Israel.
Licha ya Trump kutangaza kusitisha mashambulizi ya Marekani kwa siku tano, Netanyahu amesisitiza kuwa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) litaendelea na operesheni zake nchini Iran na Lebanon ili kuharibu kabisa uwezo wa kijeshi wa maadui zao.
Netanyahu ameeleza kuwa Trump anaamini mafanikio ya kijeshi yaliyopatikana hivi karibuni yameweka msingi mzuri wa kufikia malengo ya vita kupitia makubaliano ya kidiplomasia ambayo yatalinda maslahi muhimu ya Israel.
Netanyahu amethibitisha kuwa ndani ya siku chache zilizopita, Israel imefanikiwa kuwaangamiza viongozi wengine wawili wa ngazi za juu wa Hezbollah, jambo linalodhoofisha zaidi safu ya uongozi ya kundi hilo nchini Lebanon. Israel imeweka wazi kuwa “msitari mwekundu” ni kuhakikisha Iran haina uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia wala makombora ya masafa marefu.