Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa vita dhidi ya Iran vimeisha kwa ushindi mnono wa Marekani, huku akidai kuwa jeshi la nchi hiyo limesambaratishwa kiasi kwamba haliwezi tena kujilinda dhidi ya ndege za Marekani zinazopaa juu ya anga la Tehran.
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu ya White House, Machi 24, 2026, Trump amekishambulia kile alichokiita “vyombo vya habari vya uongo” (fake news) kama New York Times na CNN kwa kutoa taswira kuwa Iran bado ina nguvu ya kupigana.
Trump amefichua kuwa Jeshi la Maji la Iran lilifutwa kabisa ndani ya siku tatu tu chini ya usimamizi wa Waziri wa Vita, Pete Hegseth. Amedai kuwa ndege za Marekani sasa zina uwezo wa kulipua kituo chochote kikuu cha nishati nchini humo bila upinzani wowote.
“Tumeshashinda vita hivi. Iran haina tena jeshi la maji, haina jeshi la anga, na haina chochote. Ndege zetu zinapaa juu ya Tehran na hawawezi kufanya lolote. Ukisoma New York Times unaweza kudhani ni mapambano makali, lakini ukweli ni kwamba wamefutwa kijeshi,” amesema Rais Trump.
Rais huyo amesisitiza kuwa shambulio la ndege za B-2 Bombers dhidi ya mitambo ya nyuklia ya Iran lilikwepa maafa makubwa duniani. Amedai kuwa kama Marekani isingechukua hatua hiyo, Iran ingekuwa na silaha za nyuklia ndani ya wiki mbili na ingezitumia dhidi ya washirika wa Marekani Mashariki ya Kati, ikiwemo Israel, Saudi Arabia, na UAE.
Trump amethibitisha kuwa anahusika moja kwa moja katika mazungumzo ya kumaliza vita hivyo ili kuokoa maisha ya mamilioni ya watu. Ametaja timu yake ya washauri inayojumuisha Makamu wa Rais J.D. Vance, Marco Rubio, Jared Kushner, na Steve Witkoff kama viongozi wa mazungumzo hayo.
Trump amehitimisha kwa kusema kuwa lengo lake ni kuhakikisha dunia inakuwa mahali salama bila silaha za nyuklia mikononi mwa “watu hatari,” akijivunia kuwa sera zake zimeweka Marekani katika nafasi ya kipekee ya kutoa mwelekeo wa amani duniani.