Latest Posts

ZEBAKI INAVYOTUMIKA BILA TAHADHARI: WACHENJUAJI WANAJALI MIGUU KULIKO MIKONO

Na Helena Magabe, Mara.

Kuna haja kwa sekta mbalimbali zinazohusiana na madini kutoa elimu bila kuchoka kwa wachenjuaji wa madini ya dhahabu, juu ya namna sahihi ya kutumia zebaki (mercury) wakati wa uchenjuaji ili kulinda afya zao na mazingira kwa ujumla.

Inawezekana elimu imekuwa ikitolewa lakini haijawafikia wachenjuaji walio wengi, kwani wamekuwa wanatumia mikono mitupu bila kuvaa glovu (gloves), ingawa wanalinda miguu yao kwa kuvaa viatu virefu vya mpira maarufu kama ‘magambuti’.

Hivi karibuni, Jambo TV iliwakuta wanawake na baadhi ya wanaume wachache wakiwa katika shughuli ya uchenjuaji wa dhahabu katika Mgodi wa Kibaga uliopo wilayani Tarime, huku wakitumia mikono bila kuvaa vifaa kinga kama vile glovu, lakini miguuni wakiwa wamevaa viatu virefu vya mpira kwa ajili ya kujilinda kulingana na mazingira yao ya kazi.

Jinsia zote zinachenjua dhahabu, ingawa wanawake ndio wanaoonekana kuwa wengi. Wao wanachenjua kwa mikono mitupu wakidai kuwa ili “wanase” dhahabu vizuri ni lazima wafanye hivyo, licha ya kwamba wamejitahidi kujenga mialo ya kuchenjulia. Kufanya kazi wakiwa wamevaa glovu limekuwa jambo gumu, kwani wanadai zebaki haiwezi kushika dhahabu vizuri endapo watatumia vifaa hivyo.

Neema Chacha, mchenjuaji anayemiliki mwalo wake, amekuwa akifanya kazi hiyo kwa muda mrefu kwa kutumia mikono mitupu bila glovu. Anachojali zaidi ni kuvaa gambuti kujikinga na vitu vyenye ncha kali vinavyoweza kujeruhi miguu yake.

“Tunapofanya kazi hizi tunavaa viatu vya magambuti kwa ajili ya usalama wa afya zetu na kujikinga dhidi ya hatari mbalimbali zinazoweza kutokea eneo la kazi. Upatikanaji wa vifaa kinga bado ni changamoto, wachenjuaji wengi hawana glovu hivyo wanalazimika kuchenjua kwa kutumia mikono,” alisema Neema.

Aliongeza kuwa hawana elimu ya kutosha juu ya athari za matumizi ya zebaki, hivyo wanaomba wapatiwe mafunzo na teknolojia salama zaidi ili kuepuka kushika kemikali hiyo kwa mikono, jambo linalohatarisha afya zao na mazingira.

Mbali na changamoto za usalama wa kiafya, Neema alisema kuna uhaba mkubwa wa maji ya kuchenjulia dhahabu katika eneo la mialo. Hali hiyo inapelekea wachimbaji kutembea umbali mrefu kutafuta maji, jambo linalopunguza uzalishaji na kuongeza ugumu wa maisha. Aidha, alitaja gharama kubwa za ujenzi wa mialo na masharti ya makubaliano baina ya wachimbaji na wamiliki wa maeneo kuwa kikwazo kikubwa kwa wanawake wenye mitaji midogo.

Kwa upande wake, Devotha Krispin aliiomba Serikali kusaidia upatikanaji wa vifaa kinga ikiwemo glovu kwa wachimbaji wadogo ili kupunguza hatari za magonjwa na ajali za kazi. Aliongeza kuwa wauzaji wa zebaki wawapunguzie bei, kwani kiasi kidogo sana kinauzwa kwa Shilingi 10,000, bei ambayo ni kubwa kwa wachenjuaji na wachimbaji wadogo.

Naye Paschal Renatus, mchimbaji mdogo katika eneo hilo ambaye pia alikutwa akichenjua bila glovu, alisema soko la dhahabu limeathirika, hali inayowafanya wachimbaji wadogo kuuza madini yao kwa bei zisizo na tija. Alieleza kuwa gramu moja ya dhahabu yenye ubora wa juu huuzwa kwa wastani wa Shilingi 270,000, huku gramu moja ya dhahabu ya kawaida ikiuzwa kwa takribani Shilingi 250,000.

“Wachimbaji wenye leseni huuja dhahabu yao katika masoko rasmi ya halmashauri, lakini sisi wachimbaji wadogo tusiokuwa na leseni mara nyingi tunalazimika kuuza kwa walanguzi ambao hutupunguzia bei,” alisema Renatus.

Alisisitiza umuhimu wa Serikali na wadau wa sekta ya madini kuendelea kuboresha mazingira ya kazi, kutoa elimu ya matumizi salama ya kemikali, na kuwezesha upatikanaji wa vifaa kinga. Wataalamu wa mazingira wanakumbusha kuwa matumizi yasiyo salama ya zebaki yanaweza kusababisha madhara ya muda mrefu kwenye mfumo wa neva wa binadamu na kuchafua vyanzo vya maji na ardhi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!