Dereva mmoja amefariki dunia na watu wawili wamejeruhiwa baada ya lori lililokuwa limebeba tani 32 za ufuta kupinduka katika Daraja la Ingaula, Wilaya ya Kilwa, Mkoa wa Lindi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi John Imori, amesema ajali hiyo imetokea Julai 3, 2026, majira ya saa 11 alfajiri katika Barabara ya Dar es Salaam–Lindi, wakati lori hilo likitoka Masasi, Mkoa wa Mtwara, kuelekea Dar es Salaam.
Marehemu ametambulika kwa jina la Pahala (30), mkazi wa Mtwara na majeruhi ni Oliva Gerald (31), utingo wa lori na Sikuzani Chama (42), msindikizaji wa mzigo.

Kamanda Imori amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Kinyonga huku majeruhi wakiendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.
Ameeleza kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo cha ajali hiyo ni dereva kushindwa kulimudu lori alipofika kwenye kona hivyo kupinduka.
Aidha, ametoa wito kwa watumiaji wote wa barabara kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuendesha kwa tahadhari ili kuepusha ajali.
Katika tukio jingine Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi limemkamata Mayunga Peter (32), mkazi wa Somanga Wilaya ya Kilwa, kwa tuhuma za kuiba bajaji ambapo uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.