Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limethibitisha kutokea kwa tukio la mauaji ya Humphrey Elisamon Msoka (63), aliyejeruhiwa vibaya kichwani kwa panga na mtoto wa mdogo wake, kabla ya mtuhumiwa huyo naye kushambuliwa na wananchi na kufariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitali.
Tukio hilo limetokea tarehe 18 Oktoba, 2026, katika eneo la Mungu Mwema, Mtaa wa Hongoro, Kibamba Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Kulingana na taarifa rasmi iliyotolewa leo Oktoba 19, 2026 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro, marehemu Humphrey Elisamon alishambuliwa na kujeruhiwa kichwani na kijana aitwaye Dickson Elimringi Msoka (22), mkazi wa Hongoro, ambaye ni mtoto wa mdogo wa marehemu.

“Mtuhumiwa huyo baada ya tukio alishambuliwa na wananchi kabla ya Polisi kufika akiwa katika hali mbaya na baadaye alipoteza maisha akiwa anapelekwa hospitali”, ameeleza Kamanda Muliro akiongeza kuwa uchunguzi zaidi unaendelea kuhusiana na tukio hilo.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa jamii kujiepusha na tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutumia vyombo na mamlaka halali za kisheria, kijamii, kiuchumi na kidini katika kutatua migogoro.