Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu Dodoma, imeamuru kusimamishwa kwa mwenendo wa shauri la nidhamu linalomkabili Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Wakili Boniface Anyisile Mwabukusi mbele ya Kamati ya Taifa ya Mawakili, hadi shauri la kikatiba alilofungua Mahakamani hapo litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi wa mwisho.
Uamuzi huo umetolewa Oktoba 19, 2026, na jopo la majaji watatu, likiongozwa na A.R. Mruma, S.H. Hassan na Irene Musokwa, katika shauri la kikatiba namba 25918 la mwaka 2026, lililofunguliwa na Mwabukusi dhidi ya Kamati ya Taifa ya Mawakili, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwita Nashon.
Katika uamuzi wake, Mahakama imesema kusimamishwa kwa shauri hilo la nidhamu kunalenga kulinda hali iliyopo na kuzuia uwezekano wa taasisi hizo mbili zinazoshughulikia haki za wahusika kutoa maamuzi yanayoweza kukinzana, jambo ambalo lingeweza kuwa na athari kwa usimamizi wa haki nchini.
Mahakama imeeleza kuwa Kamati ya Taifa ya Mawakili ni chombo halali chenye mamlaka ya kutekeleza majukumu ya kimahakama, lakini shauri la kikatiba lililopo mbele ya Mahakama Kuu linapaswa kuamuliwa kwanza kabla mwenendo wa nidhamu haujaendelea, huku ikisisitiza kuwa kusimamishwa huko hakumaanishi upande wowote utanyimwa haki.
Wakati huohuo, Mahakama imekataa ombi la Mwita Nashon la kutaka majaji hao wajiondoe katika kusikiliza shauri hilo, ikieleza kuwa kutoridhishwa na maamuzi ya awali ya Mahakama hakutoshi kuwa sababu ya kisheria ya kuwataka majaji kujiondoa, bila kuwepo mazingira yanayoonesha uwezekano halisi wa upendeleo.
Aidha, Mahakama imekataa ombi la kutaka Mwenyekiti au mjumbe wa Kamati ya Taifa ya Mawakili aitwe Mahakamani kujieleza kuhusu madai ya kutokutii amri ya Mahakama, ikieleza kuwa madai ya dharau kwa Mahakama yaliyotokea nje ya Mahakama yanahitaji kufunguliwa kwa utaratibu rasmi, kupitia maombi yanayoambatana na hati ya kiapo inayoeleza madai hayo.
Mahakama imeahirisha shauri hilo hadi Novemba 10, 2026, saa nne asubuhi, kwa ajili ya kutajwa na kupokea maelekezo zaidi, huku amri ya kusimamisha mwenendo wa shauri la nidhamu dhidi ya Mwabukusi ikiendelea kutumika hadi shauri la kikatiba litakapoamuliwa kwa ukamilifu.