Latest Posts

LISSU AJAJWA MIONGONI MWA WATEULE 3 TUZO YA SAKHAROV

Bunge la Ulaya limetangaza wateule watatu wa mwisho (finalists) wanaowania Tuzo ya Sakharov Prize for Freedom of Thought. Orodha hiyo inajumuisha Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu, na wanawake wawili wa Iran waliohukumiwa adhabu ya kifo katika nchi yao.

Wateule hao wa mwisho wa Tuzo ya Andrei Sakharov ya Mwaka 2026 walichaguliwa na Wajumbe wa Bunge la Ulaya siku ya Jumatatu, Oktoba 19, mjini Strasbourg nchini Ufaransa. Rais wa Bunge la Ulaya, Roberta Metsola, atamtangaza mshindi rasmi tarehe 22 Oktoba.

Mahakama ya ICC, majaji wake, mawakili, na wafanyakazi wake walipendekezwa kuwania tuzo hiyo kutokana na uchunguzi wao kuhusu mauaji ya kimbari, makosa ya kivita, na makosa dhidi ya ubinadamu. Mahakama hiyo ipo chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye aliweka vikwazo dhidi ya mahakama hiyo na wafanyakazi wake, na kuagiza kuzuiliwa kwa rasilimali zao na kadi zao za mikopo nchini Marekani.

Tundu Lissu, ambaye yupo gerezani tangu mwaka 2025 na anayeongoza chama cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, yupo katika hatihati ya kukabiliwa na adhabu ya kifo kwa kosa la uhaini. Vyama vya European People’s Party (EPP) na European Conservatives and Reformists (ECR), vilivyomteua, vilifafanua uamuzi wao kwa kutaja jitihada za Lissu katika kupigania uchaguzi huru, mahakama inayojitegemea, na kukomesha ghasia za kisiasa nchini Tanzania.

Zaidi ya hayo, mabinti wawili wa tumbo moja, Taraneh na Romina Rahimi, waliohukumiwa adhabu ya kifo nchini Iran, waliteuliwa kama wawakilishi wa maandamano ya mwaka huu nchini humo. Uteuzi wao ulipendekezwa na kundi la Patriots for Europe, linalojumuisha wanasiasa wa mrengo wa kulia wa Ufaransa.

David McAllister, Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Ulaya na mwanachama wa EPP, amesema: “Kipindi hiki cha vita na ongezeko la ukandamizaji, wale wanaopaza sauti zao kwa ajili ya uhuru wanahitaji kujua kwamba wana washirika. Tuzo ya Sakharov inasaidia kufanya sauti zao zisikike. Ujasiri wao unatukumbusha kwamba haki za binadamu lazima ziongoze sera zetu za mambo ya nje, hasa pale ambapo ulinzi wake unapokuwa na changamoto za kisiasa.”

Tuzo ya Andrei Sakharov ya Uhuru wa Mawazo itatolewa rasmi tarehe 16 Desemba mjini Strasbourg, Ufaransa. Tangu mwaka 1988, Bunge la Ulaya limekuwa likitoa tuzo hiyo kwa watu binafsi na mashirika yanayotetea haki za binadamu na uhuru wa kujieleza. Zawadi ya fedha taslimu ni Euro 50,000 (takriban Shilingi za Kitanzania Milioni 145). Mwaka jana, tuzo hiyo ilitolewa kwa waandishi wa habari kutoka nchi za Belarus na Georgia.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!