Latest Posts

TANZANIA, MAREKANI WASHIRIKIANA KUPAMBANA DHIDI YA UGONJWA WA SARATANI

Tanzania na Marekani wamekubaliana kukabiliana na uhaba wa wataalamu, ukosefu wa miundombinu wezeshi, vifaa tiba hususani vya kutoa huduma za mionzi, takwimu, tafiti pamoja na ubunifu ili kuwezesha wananchi wa Afrika kupata huduma bora za saratani bila kikwazo.
 
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema hayo Jumanne tarehe 16 Julai, 2024 katika kikao kilichofanyika Ikulu ya Marekani (White House) Jijini Washington DC, Marekani ambapo ameambatana na Waziri wa Afya wa Zanzibar Nassoro Mazrui.
 
Katika kikao hicho kilichoandaliwa na Ikulu ya Marekani kupitia Taasisi ya Biden Cancer Moonshot, Waziri Ummy amesema ugonjwa wa Saratani umekuwa ni changamoto kubwa nchini Tanzania ambapo inakadiriwa uwepo wa ongezeko la wagonjwa wapya wa saratani takribani 45,000 kila Mwaka.
 
“Ugonjwa huo wa Saratani unapelekea vifo elfu 29,743 ambayo ni sawa na asilimia 66 kwa mwaka, uwepo wa vifo vingi vitokanavyo na ugonjwa huu nchini Tanzania ni kwa sababu wananchi wengi huchelewa kugundulika kuwa na saratani na ukosefu wa huduma za matibabu ya saratani kwa wananchi.” Amesema Waziri Ummy
 
Waziri Ummy amewashukuru waandaaji wa mkutano huo ambao ni Taasisi ya Biden Cancer Moon shot na Taasisi ya International Atomic Energy kwa kuamua kushirikiana na nchi za Afrika katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa saratani ili kuokoa maisha ya wengi.
 
Kwa upande wake, Mratibu wa Bi. Catherine Young kutoka Taasisi ya Biden Cancer Moonshot wakati akifungua mkutano huo amesema Taasisi hiyo imeandaa kikao hicho muhimu kwa ajili ya kuwaleta pamoja wadau wakubwa wanaojishughulisha na ugonjwa wa Saratani ili kuwezesha Afrika kupambana vyema na ugonjwa wa Saratani.
 
Taasisi hiyo imeahidi ongezeko la kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 10 karibu na bilioni 300 za Kitanzania ambazo zitasaidia katika mapambano ya ugonjwa wa Saratani hususani katika nchi za Afrika.
 
Naye Mkurugenzi wa masuala ya UKIMWI katika ofisi ya Rais Ikulu ya Marekani, Balozi John Nkengasong amesema ni wakati muafaka sasa kuwekeza katika afua za kinga, mafunzo pamoja na utafiti katika magonjwa ya Saratani.
 
Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa Sekta ya Afya kutoka nchi nane za Afrika ikiwamo Tanzania, Sierra Leone, Rwanda, Benin, Zambia, Congo DRC, Lesotho pamoja na Msumbiji.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!