Na Josea Sinkala, Songwe.
Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo mkoa wa Songwe Elia Zambi, ametangaza nia ya kugombea ubunge jimbo la Mbozi mkoani Songwe kupitia chama hicho na kuahidi kuwapigania wakulima ili kuona tija kwenye kilimo tofauti na sasa ambapo kilimo imekuwa kama mateso.
Zambi amesema hayo wakati akizungumza katika mji wa Mlowo wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, ambapo amesema Chama Cha Mapinduzi kimekuwa na ahadi hewa kwa wananchi hususani kuhusu ubovu wa barabara za jimbo hilo.
Amesema ameomba kuwania ubunge jimbo la Mbozi kwa mwaka 2025 ikiwa chama hicho Taifa kitatangaza kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu ili kuhakikisha anapigania mabadiliko ya kweli kwa wananchi.
Ameeleza kero kubwa zilizomsukuma kuomba kuwania nafasi hiyo kuwa ni ubovu wa barabara na mitaani na barabara kubwa ya kutoka Mlowo Itaka hadi Utambalila na Kamsamba wilayani Momba kuendelea kuahidiwa bila utekelezwaji wowote kwa zaidi ya miaka ishirini na wakulima kuendelea kulima kilimo kisicho na matokeo halisi kutokana na bidhaa za kilimo kuwa ghari.
Pamoja na hayo amesema ACT Wazalendo inaendelea kushinikiza marekebisho ya sheria na tume huru ya uchaguzi.