Tanzania imeombwa kuonesha uongozi wa dhati katika kushughulikia mgogoro wa baada ya uchaguzi mkuu nchini Msumbiji, ambao umeibua maandamano makubwa na vifo vya mamia ya raia.
Hayo yamebainishwa na Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa chama cha ACT Wazalendo, Dkt. Nasra Nassor Omar katika taarifa ya chama hicho ya siku ya Alhamisi Desemba 26, 2024. ACT imesisitiza kuwa machafuko haya yana athari za moja kwa moja kwa usalama na ustawi wa Tanzania, hasa katika mikoa ya kusini inayopakana na Msumbiji.
“Kama majirani wenye historia ya pamoja ya harakati za ukombozi, Watanzania na Wamsumbiji wana uhusiano wa kina. Ni jambo lisilokubalika na dhuluma kubwa kubaki kimya huku Msumbiji, taifa ambalo Tanzania inashiriki nalo mpaka wa zaidi ya kilomita 850, likikabiliwa na machafuko makubwa”, imeeleza taarifa hiyo.
Mgogoro wa Msumbiji umeibuka baada ya matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 15, 2024, kukataliwa na upinzani kwa madai ya udanganyifu. Maandamano yaliyofuata yamesababisha vifo vya mamia ya watu, huku mauaji ya kisiasa yakiendelea, likiwemo la mkuu wa idara ya ujasusi ya taifa.
Katika wito wake, ACT Wazalendo imeitaka Serikali ya Tanzania kuongeza juhudi za kuhakikisha usalama wa mipaka, kuzuia biashara haramu ya silaha, na kulinda wananchi wa Tanzania waliopo Msumbiji. Chama hicho pia kimehimiza hatua za kidiplomasia za kuleta mazungumzo jumuishi kati ya wadau wa kisiasa nchini Msumbiji.
Huku Tanzania ikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya SADC ya Ulinzi, Usalama, na Siasa, ACT Wazalendo imeitaka nchi hiyo kuhakikisha SADC inachukua hatua za haraka kushughulikia mgogoro huo. Viongozi wa Afrika pia wametakiwa kuonesha mshikamano wa kweli na wananchi wa Msumbiji, huku Umoja wa Afrika (AU) ukihamasishwa kuunga mkono suluhisho la kudumu kwa mgogoro huo.
ACT Wazalendo imesema kuwa machafuko zaidi nchini Msumbiji yanaweza kuleta athari za kiusalama kwa Tanzania, ikiwa ni pamoja na wimbi la wakimbizi na changamoto za kiusalama kwa jamii za mikoa ya Mtwara, Lindi, na Ruvuma.
Katika taarifa taarifa hiyo, ACT imesisitiza kwamba Tanzania inawajibika kutumia nafasi yake ya uongozi kikanda kuleta amani Msumbiji. Aidha, imeongeza kuwa ACT Wazalendo iko tayari kushirikiana na taasisi nyingine ili kuhakikisha haki na amani vinapatikana nchini Msumbiji.