Latest Posts

AINA MPYA YA MAGUGU MAJI YAGUNDULIKA ZIWA VICTORIA

ANANIA KAJUNI

Aina mpya ya magugu maji jamii ya Salvinia SPP yamegundulika katika Ziwa Victoria, yakisababisha changamoto kubwa kwenye sekta ya uvuvi, usafiri wa maji, na mazingira.

Magugu maji hayo yana uwezo wa kuzaliana mara mbili hadi tatu kila baada ya siku nane (8), yanazidi kuenea kwa kasi katika maeneo mbalimbali kando ya ziwa hilo huku yakileta madhara makubwa kiuchumi na kimazingira.

Akizungumza leo na Waandishi wa Habari ofisini kwake Meneja Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Ziwa Victoria, Jarome Kayombo amesema aina hiyo mpya ya magugu maji ilianza kuonekana katikati ya Agosti 2024 katika maeneo ya Buyagu (Wilaya ya Sengerema), Chole, Nyahiti, na Mbarika (Wilaya ya Misungwi).

Kayombo amesema kufuatia upepo na mienendo ya maji, magugu maji hayo yameenea haraka hadi kufikia maeneo ya Kigongo-Busisi, yakiathiri shughuli za uvuvi, ufugaji samaki, na usafiri wa maji.

“Wataalamu wamebainisha kuwa ongezeko la virutubisho ndani ya Ziwa Victoria, linalosababishwa na shughuli za kibinadamu kama vile kilimo, utupaji wa taka majini, ujenzi wa makazi, na shughuli za uchimbaji madini, ndizo sababu kuu za kuenea kwa magugu haya. Shughuli hizi, ambazo hazizingatii misingi ya utunzaji endelevu wa mazingira, zimeongeza kiwango cha virutubisho vya majini, hivyo kuifanya Salvinia spp kuenea kwa kasi,”.

Amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali kama Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB), Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) na taasisi nyingine, zimeunda kikosi maalum cha kukabiliana na janga hilo.

“Kikosi hiki kimefanya kazi kubwa ikiwemo kubaini aina ya magugu, tabia zake, na maeneo yaliyoathirika. Kufikia sasa, zaidi ya tani 36 za magugu zimeondolewa katika eneo la Kigongo-Busisi,” amesema.

Kayombo amesema magugu hayo ni hatari kwa maisha ya viunbe hai majini kutokana na kuzuia upatikanaji wa oksijeni, kuharibu mifumo ya ikolojia, kuathiri shughuli za uvuvi, ufugaji samaki kwa njia ya vizimba na upatikanaji wa maji safi na salama.

Kayombo mbali na kuwapa pole waathirika wa magugu hayo amesema tayari NEMC wameanzisha mipango ya muda mfupi, wa kati na mrefu kukabiliana na changamoto hiyo huku pia wawekezaji wote wakitakiwa kuzingatia sheria za mazingira ili kuzuia uchafuzi wa Ziwa Victoria na kuhakikisha maendeleo endelevu.

“Baraza linatoa wito kwa wadau wote, ikiwemo serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wananchi, kushirikiana katika jitihada za kutokomeza magugu haya,” amesema.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!