Na Josea Sinkala, Mbeya.
Kutokana na ajali iliyoua watu wanne akiwemo mwandishi wa habari mkoani Mbeya, Chama cha waandishi wa habari mkoa wa Mbeya (Mbeya Press Club – MBPC) kimeitaka Serikali kuwashinikiza wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha waandishi wa habari wanapewa bima za afya ili kuwahakikishia usalama wa afya zao.
Pamoja na hayo, Mbeya Press Club imeitaka Serikali kuwajali wanahabari kwa kuhakikisha wanapokuwa na ziara wapewe magari yaliyothibitika kuwa imara ili kuwaepusha na madhira ambayo wamekuwa wakikumbana nayo mara kadhaa wakati wa utekelezaji majukumu yao hasa wawapo kwenye misafara ya viongozi wa kiserikali.
Chama hicho cha kitaaluma cha mhimili wa nne usio rasmi kimesema hakuna sababu ya kuharakisha au kuwa na mwendo mkali wa madereva wa Serikali bila sababu za msingi hivyo kuitaka Serikali kupitia mamlaka zake kusimamia masuala hayo, maombi yaliyotolewa na mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari mkoa wa Mbeya Nebart Msokwa kwa niaba ya wanahabari mkoani humo.
Pamoja na kuomba wamiliki wa vyombo vya habari kuwapatia bima za afya watumishi wake, pia Msokwa ameeleza kusikitishwa kwake na kifo cha mwandishi wa habari wa kujitegemea Furaha Simchimba na waandishi wengine watatu kujeruhiwa na kwamba wanaendelea na matibabu katika hospitali ya rufaa ya kanda Mbeya.
Mpaka jumatano hii (Februari 26, 2025) jumla ya watu wanne walikuwa wamethibitika kufariki Dunia kutokana na ajali iliyotokea Februari 25, 2025 huko katika kijiji cha Shamwengo Mbeya vijijini wakati wakirudi kwenye msafara na viongozi wa Chama (CCM) na Serikali walipokuwa wakitoka kumsindikiza Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wa CCM Taifa Fadhil Maganya baada ya kuhitimisha ziara yake mkoani Mbeya na kukabidhiwa mkoani Njombe.
Taratibu za maziko kwa mwili wa mwandishi wa habari Furaha Simchimba zinaendelea kufanyika na familia yake kwa kushirikiana na waandishi wa habari mkoani Mbeya.