Latest Posts

AMBULANCE YALETA NEEMA KWA WANANCHI ILULA

 

Kituo cha Afya cha Ilula Masukanzi kimepokea gari jipya la kubebea wagonjwa (ambulance), ambalo litatumika katika zahanati na vituo vya afya vya tarafa ya Mazombe na Mahenge, Wilaya ya Kilolo, Mkoani Iringa.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi gari hiyo, Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Mhe. Justin Nyamoga, alitoa shukrani kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuboresha huduma za afya.

Aidha Nyamoga ametoa wito kwa watumishi wa afya kuhakikisha gari hiyo inawasaidia wananchi wanyonge wasiokuwa na uwezo kwani ndio madhumuni yake na si vinginevyo .

Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Bi Anna Msola, amewaomba wananchi wa Kata ya Ilula kuonyesha ushirikiano na umoja katika kuwasaidia watumishi wa kituo hicho ili kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kuboreshwa.

Awali, Tabibu wa Meno katika Kituo cha Afya Ilula, Rachel Haule, alisema kuwa gari hilo ni la tatu kupokelewa Wilayani Kilolo, lakini ni la kwanza kupokelewa katika Kituo cha Afya Ilula.

Wakazi wa Ilula, walieleza furaha yao baada ya kituo hicho kupokea msaada wa gari la kubebea wagonjwa, wakisema kuwa wataepukana na changamoto za usafiri wa haraka pindi mgonjwa anapohitajika kupelekwa kwenye hospitali kubwa.

Hafla ya makabidhiano ya gari hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa Serikali ya Wilaya, wananchi, na watumishi wa afya wa Kituo cha Afya Ilula.

Hata hivyo gari hilo litaendelea kusimamiwa na kituo hicho ili kutoa huduma kwa wananchi wa kata hiyo na maeneo jirani.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!