Nelson Amenya aliyezua hali ya taharuki baada ya kufichua mazungumzo ya siri ya kampuni ya Kihindi kuchukua Uwanja wa Ndege Mkuu wa Kenya amesema kuwa kwa sasa hana majuto, lakini anahofia maisha yake yako hatarini, kulingana na Shirika la habari la AFP.
Nyaraka ambazo Amenya alishiriki mtandaoni mwezi Julai zilionesha kuwa Adani Group, inayomilikiwa na Gautam Adani, tajiri mkubwa zaidi wa India, ilikuwa imefanya mazungumzo kwa miezi kadhaa ili kuuchukua na kuusimamia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa miaka 30.
JKIA ni moja ya viwanja vya ndege vilivyo na shughuli nyingi zaidi barani Afrika, lakini mara nyingi hukumbwa na kukatika kwa umeme, paa zinazovuja na inahitaji sana kufanyiwa ukarabati.
Adani ilitoa pendekezo la uwekezaji wa dola bilioni 1.85, lakini wakosoaji wanasema hiyo ni kidogo ikilinganishwa na umuhimu wa kimkakati wa uwanja huo wa ndege, ambao ada zake huchangia asilimia tano ya Pato la Taifa la Kenya.
Mazungumzo hayo yalifanyika kwa usiri mkubwa bila juhudi zozote za kuwaita wazabuni wengine.
“Hawakutaka yafahamike kwa umma kwa sababu ya masharti. Adani alitaka kuweka asilimia 18 ya umiliki wa uwanja huo hata baada ya mkataba wa miaka 30 – hii ni upuuzi,” Amenya aliiambia AFP.
Ufichuzi wake ulisababisha mgomo wa wafanyakazi wa uwanja wa ndege na uchunguzi kamili wa bunge.
Akiwasilisha ushahidi wiki iliyopita, Waziri wa Fedha wa Kenya John Mbadi, ambaye ameanza hivi karibuni kushika wadhifa huo, alikiri kushangazwa kugundua kuwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Kenya (KAA) ilikubali pendekezo la Adani chini ya siku moja mnamo Machi.
KAA haijatoa maoni juu ya usiri wa mpango huo, lakini iliahidi kuwa itapitia tathmini za kitaalamu, kifedha, na kisheria pamoja na taratibu zinazohitajika.
AMENYA ASEMA HAYUKO SALAMA
Badala ya kusifiwa kwa kufichua mpango huo kwa umma, Amenya anasema anashambuliwa kwa njia nyingi.
Mara baada ya kufichua mpango huo, Idara ya Upelelezi wa Jinai ya Kenya iliandika kwa kampuni ya kaboni ambayo aliianzisha, ikiwashtaki kwa kuuza sarafu bandia za kidijitali.
“Hatuuzi sarafu za kidijitali, hatufanyi biashara kwenye tovuti yetu kabisa,” Amenya alisema kwa kicheko.
Alikubali kufichua mpango huo kwa sababu anasoma Ufaransa kwa sasa. “Kama ungekua Kenya, ungetishiwa na polisi, mamluki, au hata kupoteza maisha. Ninajua siko salama na ninaweza kuuawa wakati wowote nikiwa Ufaransa,” alisema Amenya. Hakutaka kutoa maelezo kuhusu vyanzo vyake, lakini amepeleka wasiwasi wake kwa polisi wa Ufaransa.
“Unazungumzia mpango wa dola bilioni 2 na hujui ni kiasi gani cha pesa kimebadilishana mikono hadi kufikia hatua hii,” aliongeza.
Kinachompa wasiwasiAmenya zaidi kuhusu mpango huo wa uwanja wa ndege ni sifa ya Adani.
Kampuni hiyo kubwa ya Kihindi inayohusisha bandari hadi nishati ilipoteza thamani ya dola bilioni 150 mwaka jana baada ya ripoti ya Hindenburg Research, kampuni ya uchunguzi ya Marekani, kuishutumu kwa “udanganyifu wa hisa na udanganyifu wa kibenki.”
Wanaharakati wa mazingira wa Australia wanaituhumu kampuni hiyo kwa “uharibifu wa mazingira, ukiukaji wa haki za binadamu, ufisadi, na mikataba haramu” kuhusiana na shughuli zake za madini huko.
Adani inaishtaki mkosoaji wake mkuu, Australia na inasema ripoti ya Hindenburg ilikuwa “shambulio la makusudi la kuharibu sifa yake.”
Amenya anaamini mpango wa uwanja wa ndege usingekuwa hadharani hadi uwe umetiwa saini, kama asingelifichua.
“Ulikuwa wakati sahihi kufanya hivyo kwa sababu walikuwa karibu kusaini makubaliano ya kibiashara na kuanza hatua ya maendeleo ya mradi,” alisema Amenya.
“Tunaweza tusifanikiwe kuzuia Adani kuchukua JKIA, lakini angalau tunaweza kushawishi masharti.”
Serikali ya Kenya inasema masharti bado yanajadiliwa na kuwa ukarabati wa uwanja wa ndege ni muhimu.