Latest Posts

AMNESTY: MFUMO WA MISAADA GAZA UMEGEUZWA MITEGO YA KIFO

Mashambulizi makali ya anga yanayoendelea kufanywa na jeshi la Israel yameripotiwa kuua zaidi ya Wapalestina 300 ndani ya saa 48 zilizopita, wengi wao wakiwa wamesimama kwenye foleni za chakula karibu na vituo vya misaada katika Ukanda wa Gaza.

Taarifa za mashirika mbalimbali zinasema vifo hivyo vimetokea karibu na vituo vya Wakfu wa Kibinadamu wa Gaza (GHF), ambavyo vimekuwa vikituhumiwa na mashirika ya haki za binadamu kwa kushindwa kutoa misaada ya kibinadamu kwa usalama na kwa njia ya heshima kwa raia.

Shirika la haki za binadamu la Amnesty International limeitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua dhidi ya kile ilichokiita “matumizi ya njaa kama silaha ya kivita” na “mfumo wa misaada usio wa kibinadamu unaoendeleza mauaji ya kimbari.”

“Israel imegeuza maeneo ya misaada kuwa mitego ya kuwanasa na kuwaua Wapalestina wanaosaka chakula,” alisema Agnes Callamard, Katibu Mkuu wa Amnesty International.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, zaidi ya watu 500 wameuawa ndani ya mwezi mmoja uliopita wakiwa ama ndani au karibu na vituo vya GHF, ambavyo vinadaiwa kuwa karibu na maeneo ya kijeshi ya Israel.

Wapokeaji misaada na mashuhuda wameripoti kuwa wamekuwa wakilengwa kwa risasi na walinzi wa kampuni binafsi au wanajeshi wa Israel wanapojaribu kupata chakula. Hata hivyo, wakfu wa GHF umekanusha kuwa na walinzi wenye silaha, ukisema milio ya risasi inayosikika ni kutoka kwa jeshi la Israel.

Katika hali hiyo ya sintofahamu, Israel imejibu kwa kukana ripoti hiyo ya Amnesty International, ikisema ni propaganda inayoratibiwa na wafuasi wa Hamas.

Mashirika zaidi ya 160 ya misaada ya kimataifa yameungana na Amnesty kutaka shirika la GHF lisitishwe mara moja kwa madai kuwa mfumo wake unakiuka misingi ya misaada ya kibinadamu na hauna ufanisi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!