Katika juhudi za kuimarisha sekta ya ufugaji na kuboresha ustawi wa jamii, kampuni ya Asas imetekeleza ahadi yake iliyotolewa wakati wa Sherehe za Kizimkazi Festival kwa kuandaa ziara ya wafugaji kutoka Kizimkazi kwenda kwenye mashamba yake yaliyopo Iringa.
Itakumbukwa mnamo Agosti 8, 2024 kampuni ya Asas iliahidi kuwapa wafugaji wa Kizimkazi fursa ya kujifunza mbinu za kisasa za ufugaji katika mashamba yake.
Sasa hatimaye ahadi hiyo imetekelezwa na Mwakilishi wa kampuni ya unywaji na uuzaji wa maziwa ya Asas akieleza namna wafugaji wa Kimzikazi walivyopata elimu na fursa juu ya ufugaji.
“Kama utakumbuka kwenye Sherehe za Kizimkazi Festival tuliahidi kuwaleta wafugaji wa Kizimkazi katika mashamba yetu na hatimaye tumetekeleza, na ziara hii kwa wafugaji hawa imetufungulia macho, na maarifa mapya ambayo yakitumika vizuri yatasadia kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha yetu”, amesema msemaji huyo wa kampuni ya Asas.
Aidha amesema kuwa wakati wa ziara hiyo, wafugaji wamejifunza mifumo ya kisasa ya malisho, mbinu za matibabu ya mifugo, na usindikaji wa maziwa. Aidha, wamepewa elimu juu ya jinsi ya kuboresha uzalishaji na kudumisha afya ya mifugo kwa njia endelevu.
Msemaji huyo ameongeza kuwa utekelezaji wa ahadi hii ni sehemu ya mkakati wa uwajibikaji wa kijamii wa Kampuni ya Asas.
“Kwa miaka mingi, Asas imekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono maendeleo ya kilimo na ufugaji, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa uwajibikaji wa kijamii. Utekelezaji wa ahadi hii unadhihirisha dhamira ya dhati ya kusaidia wafugaji wadogo ili kuongeza kipato na kuboresha maisha yao”, amesema.
Asas imeonesha kuwa sekta binafsi inaweza kuchangia maendeleo ya kijamii kwa vitendo kupitia uwekezaji katika elimu na mafunzo kwa jamii za wafugaji. Kampuni hiyo imejizatiti kuendelea kushirikiana na wafugaji wa maeneo mbalimbali ili kuboresha sekta ya ufugaji nchini.