Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, Aaron Kagurumjuli, amesema halmashauri hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha maslahi ya watumishi wote wa umma yanalindwa kwa kuwapatiwa stahiki zao kwa mujibu wa mipango na bajeti iliyopitishwa.
Kagurumjuli ametoa kauli hiyo Januari 6, 2026 Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika kikao cha wadau wa watumishi wa umma, ambapo ameeleza kuwa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 imezingatia mahitaji halisi ya wafanyakazi na wananchi kwa ujumla.

Amesema bajeti hiyo imelenga kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na kusukuma mbele utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya Manispaa ya Ubungo, huku akisisitiza kuwa usimamizi makini wa fedha umepewa kipaumbele.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Waalimu Manispaa ya Ubungo, Mwl. Sostenence Haule, amesema kikao hicho kimefanyika kwa lengo la kupitia bajeti ya 2025/2026 na kutoa ushauri kuhusu maeneo yanayogusa moja kwa moja maslahi ya watumishi wa umma.
“Bajeti hii imekidhi mahitaji na matarajio ya wananchi pamoja na wafanyakazi. Imezingatia maeneo yote muhimu na imefungua fursa nyingi zenye tija kwa halmashauri yetu,” amesema Haule.

Haule ameongeza kuwa watumishi hawapaswi kuwa na wasiwasi juu ya utekelezaji wa bajeti hiyo, akibainisha kuwa Manispaa ya Ubungo imepata ongezeko kubwa la mapato ya ndani ikilinganishwa na miaka ya nyuma, hali itakayowezesha utekelezaji wa miradi yote kwa wakati.
Naye Kiongozi wa Wafanyakazi na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALB) Dkt. Ally Njama, amesema bajeti iliyowasilishwa ina afya na ina uwezo wa kutatua changamoto nyingi zinazowakabili watumishi wa Manispaa ya Ubungo.
Dkt. Njama amesema bajeti hiyo imegusa maeneo muhimu ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, barabara pamoja na stahiki za watumishi kama mafunzo na malipo ya likizo, akieleza kuwa utekelezaji wake unatarajiwa kwenda vizuri.
Kwa ujumla, wadau wa sekta ya umma ameeleza matumaini makubwa kuwa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 itakuwa chachu ya maendeleo, itaboreshwa ustawi wa watumishi wa umma na itaongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi wa Manispaa ya Ubungo.